Tuesday, December 26, 2023

NG'WANA MABINA.


  NG'WANA MABINA


"Sura ya Kwanza"

(1)

Nyambiti.

Nyambiti ni mahali penye historia yake kwa sisi  wazawa. Wazazi wangu ni baadhi ya wazawa wa mahali hapo. Nilipokuwa na umri wa kutambua kitu na kutunza kumbukumbu, mengi yalizungumzwa na mengi niliyashuhudia kwa macho yangu mwenyewe.

Makuzi yangu yalikuwa ni ya kawaida tu, ila nilikuwa ni mtafiti wa kila niliposikia ama kuona kioja, basi ilinichukulia muda kutafuta ni nini kilicho zungumzwa au kutendeka.

Mimi ni mzaliwa wa pili kwa mama ila ni mzaliwa wa tatu kwa baba. Nina maana kwamba, kabla mama hajaolewa na baba, baba alikuwa na mwanamke mwingine ambaye alimzalia mtoto wa kike. Alipomuoa mama, alimzalia mtoto wa kwanza wa kike ndipo nikafuata mimi na kisha wa mwisho alikuwa ni wa kike. 

Enzi hizo wazazi walikuwa na utaratibu, mmoja, baada au kabla ya chakula cha jioni; watoto tulikusanyika mbele ya wazazi kuwasikiliza simulizi zao, baadhi zikiwa ni mafundisho na maonyo nakadhalika. Kipindi hicho nilikuwa napenda sana kusikiliza hadithi kwani, mengi liyafahamu kutokana na simulizi za wazazi wangu. Nilikuwa msumbufu sana wa kuuliza maswali mbalimbali, mwishowe walinipa jina la 'Song'hwe'. Ni jina la ndege ambaye hushambulia sana mpunga unapokuwa shambani, ana kelele sana. Hivyo waliifananisha na ndege huyo.

Siku moja wakati tunasikiliza  simulizi ambayo alikuwa anatusimulia baba yetu. Aliongea kitu ambacho kilipelekea nimuulize swali. Nilimuuliza kuhusu ukoo wake walitokea wapi?

Baba alinijibu kuwa, Babu yake yeye, alitoka katika kisiwa cha Ukerewe kilichopo ziwa Victoria. Babu yake huyo alihamia hapo Nyambiti akiwa na wake zake watatu.

Mke wa kwanza alimzalia watoto watatu wote wa kiume. Mmoja alimpa jina Mashilungu, mwingine Nyanda na wa mwisho alimwita Gwanchelle.

Mke wa pili, alimzalia watoto wanne, watoto watatu wa kiume na mmoja wa kike. Mtoto wa kwanza alimwita kwa jina la Maballa aliyefuatia alimwita Sekeyi, mwingine Lubella na wà mwisho alimpa jina la Nyanzalla.

Mke wa mwisho alimzalia mtoto mmoja tu wa kike ambaye alimpa jina la Nkemachu. Babu yake huyo alijulikana kwa jina la WIGAYI IBESSE. Alikuwa ni muumini wa dini ya Kiislamu kwa jina aliloitwa HUSSEIN.

Baba aliendelea kunisimulia kuwa, Wigayi alipofariki mwili wake ulihifadhiwa maeneo ya relini mahali uliopo kuwa mji wake, maarufu kama Gengeni. Familia yake ilisarambatika baada ya kifo chake. Gwanchele mtoto wa kwanza wa mke wa kwanza alichukua urithi wa mali ilyopelekea kutokea mtafaruku kati yake na Nkemachu ambaye ni dada yake, kwa mke wa mwisho wa Wigayi.

Mashilungu aliondoka Nyambiti na alihamia Ntunzu ya Lugulu Shinyanga. Huko alioa mke aliyemkuta tayari ana watoto. Katika maisha yake hakuwahi kumzalia mtoto hata wa dawa. Mwisho wa maisha yake ulikuwa hapo hapo Ntuzu ya Lugulu.

Baba alizidi kunisimulia kwamba. Mali zake zilirithiwa na watoto wa kulea, hata hivyo hayakuwa matakwa yao, bali yalikuwa ni maamuzi ya baba yangu ambaye ni mtoto wa mdogo wake.

Lubella na Nyanzalla ambao ni watoto wa mke wa pili, wao walihama. Lubella alihamia Innala na Nyanzalla alihamia mjini Mwanza.

Hawa wengine wote walibaki Nyambiti. Sekeyi aliishi mashariki ya Nyambiti barabara iendayo Malya kupitia Goloma. Maballa aliishi jirani sana na nyumbani kwa baba yangu. Nkemachu yeye aliishi nyuma ya mlima kwa upande wa pili kwa sasa kuna Kanisa. Kwa upande magharibi wa mlima huo, ndipo kuna makaburi ya baadhi ya familia ya WIGAYI IBESSE (HUSSEIN).

Nyanzalla alimzaa Maige na Lugugumila. Mimi sijui niwaite hao ni baba zangu. Nadhani itakuwa hivyo. Kama nimekosea, wasomaji watanisahihisha. Huyo mama yao ambaye ni Nyanzalla kwangu mimi atakuwa ni bibi yangu. Kwa sababu hata huyo Nkemachu nilikuwa namwita bibi, baba alikuwa anamwita Shangazi.

Hivyo basi, mmoja wa watoto wa Wigayi Ibesse alikuwa ni baba wa baba yangu aliitwa Nyanda kwa jina la kiimani aliitwa Salum. Huyu Nyanda ama Salum mkewe ndiye aliyemzaa baba yangu, kwa jina aliitwa Mabina ama Shaban.

Ndiyo kusema Nyanda ama Salum, alikuwa ni babu yangu, mkewe alikuwa ni bibi yangu. Alifahamika kwa jina la Ng'wana Kakela au Nenwa/Nenije ama Aisha. Alikuwa mpezi wa pombe ya kienyeji aina Kangara au Swezo na alikuwa mbwia tumbaku nikiwa na maana ugoro.

Baba alikuwa na dada zake wawili ambao ni shangazi zangu. Wote wawili walikuwa na maumbo makubwa, wamepanda juu, rangi yao ilikuwa ni ya kiarabu. Mmoja aliitwa Gwalihwa ama Johari, wa pili Nyieji ama Zainab. Ndugu hawa walikuwa wanapendana sana, ila hawakufanikiwa kupata watoto, wala hawakuwahi kutumia kilevi cha aina yoyote ile.

Sifa za shangazi zangu, baba yangu na hata bibi yangu, nilizishuhudia kwa macho yangu wenyewe sikusimuliwa na yeyote. Baba pekee ndiye aliyenisimulia habari ya familia yake ilikotoka.

Majina haya mara nyingi huwa na historia yake au maana yake. Nikianza na jina la kiongozi wa familia yaani WIGAhYI IBESSE, Wigayi peke yake lina maana ya asiyetaka usumbufu, kero, unafiki. Ni mpenda amani zaidi. Ibesse lina maana ya kitu kingali hakijafanyiwa kazi, tunda lililo bivu, chakula ambacho hakijaiva. Hivyo basi alikuwa na ni mtu asiyependa kero na alipenda kumaliza jambo likiwa bado halijakomaa, bado bichi.

Tukija kwa hawa watoto zake, tukianzia na Mashilungu. Huwa kuna vifaa furani vya kiutamaduni huvaliwa katika mambo ya kimizimu. Kikiwa kimoja huitwa Shilungu vingi ni Mashilungu. Inawezekana basi huenda wakati anazaliwa alilazimika kuvaa vifaa hivyo pamoja na wakunga wake. Si unajua enzi za huko nyuma,  huduma zilikuwa ni za kienyeji asilimia kubwa.

Nyanda lina maana ya kijana mdogo. Yawezekana kuzaliwa kwake kulikuwa na vijana wadogo walio toa msaada kwa namna moja au nyingine, wakati alipokuwa anajifungua.

Jina hili la Gwanchele/Gwamchele, lina maana ya kwamba, yaani kila uchao ni ubwabwa au wali. Mchele kwa matumizi ya lugha zetu zingine unapokuwa umepikwa huitwa mchele hivyo hivyo badala ya wali au ubwabwa. Hivyo basi nyakati mama yake alipokuwa na uja uzito wake, alichunuku sana kila uchao yeye ni ubwabwa/wali. Hivyo alipojifungua mtoto akaitwa jina hilo.

Tukija kwenye jina la Maballa, hili lina maana ni eneo la ardhi ambalo lipo wazi lilisilo na mazao, lenye sura ya kama barabara vile, pia lina urefu mkubwa wa kutoka kijiji hadi kijiji. Ndiyo kusema, mama alishikwa uchungu akiwa katikati ya eneo hilo na akajifungua. Hapo ndipo mtoto akapatiwa jina hilo.

Seeke/Seekeyi. Lina maana ya kuchekwa, mchekwa, au uchekaji. Mama huyu alipokuwa mja mzito, kwa nmna moja au nyingine aitha kulikuwa na mabezo fulani ya uja uzito wake. Si unajua tabia zetu binadamu za kukaa wawili watatu au zaidi, kisha mnamjadili mtu na kushusha kicheko kile cha macho upande. Mungu alipomjalia kujifungua mtoto, akampa jina hilo.

Jina Lubella lina maana ya kupendeza aitha kwa mavazi ama mapambo ya mwilini. Huenda jina hilo alipewa kutokana na mama yake alivyokuwa na umaridadi katika mbio zake za uja uzito.

Nyanzalla lina maana ya kutotosheka na chakula. Kila mara yeye hudai ana njaa. Hapa inawekekana wakati wa uja uzito, yeye alikuwa kinjaa njaa. Kwa upande mwingine alizaliwa kipindi cha njaa na kupewa jina hilo.

Nkemachu, lina maana kuwa, mwanamke ni kiangazi, ukimtaka mwanamke mzuri utampata wakati wa kiangazi. Kwa upande mwingine alizaliwa kipindi cha kiangazi kikali, wakampa jina hilo.

Ng'wana Kakella, Kakella lina maana ya Kuvuka mahali kama mto, mfereji nakadhalika. Inawezekana wakati wa kujifungua mama yake huyo alikuwa katika harakati za kuvuka mto.

Nyieji, jina hili lilitokana na utembezi, mtu asiye tulia sehemu moja. Uja uzito wake yaelekea alikuwa ni mtu sio wa kutulia, alikuwa mzururaji, na hata muda wake wa kujifungua ulimfumania akiwa matembezini.

Gwalihwa, maana yake ni kila uchao ni mlo. Ndani ya uja uzito wake kila uchai yeye alilolifanya ilikuwa ni kutafuta mulo.

Mabina, jina hili lina maana ya michezo ya ngoma, furaha,  na burudani. Ila jina hili lina historia yake kubwa. Ni jina ambalo hakupewa na wazazi bali jina hilo lilifanywa kununuliwa na mwana Nzengo mmoja.

Huyu Nyanda baada ya kumuoa mke wake, kwa mujibu wa maelezo aliyonisimulia bibi yangu.  Mumewe alichukuliwa kujiunga na Jeshi la Kikoloni "K.A.R" (King African Rifle). Katika vita ya kwa ya dunia alikuwa ni mmoja wa aliyekuwa mstari wa mbele wa vita hivyo nchini Barma. Famila yake ilibaki Kambini kwenye mahandaki huko Alujoro Arusha. Mkewe alimwacha akiwa ana uja uzito wa huyo Mabina. Hivyo basi alizaliwa kipindi cha mwisho mwisho wa vita hiyo.

Baada ya vita kumalizika, wote waliokuwa vitàni walipewa mapumziko. Babu huyo aliondoka na mkewe pamoja na mtoto wao hadi kijijini Nyambiti. Walipokelewa kwa furaha na shangwe. 

Ulikuwa ni muonekano mpya kwa wana kijiji kumuona mtoto aliyezaliwa chini ya handaki, pia wakati baba yake alikuwa vitani. Ilikuwa ni moja ya maajabu. Chukulia nyakati hizo mambo mengi ya nchi zilizokuwa zimeendelea yalionekana ni maajabu kwa nchi zetu za kiafrika.

Mwana nzengo mmoja, kwa furaha na upendo mkubwa aliomba ampe jina kwa kulilipia kwa gharama ya ng'ombe mmoja. Ombi lake lilipo kubaliwa ilifanyika sherehe kubwa. Enzi hizo, ukiwa na rafiki ni rafiki kweli kuliko hata nduguyo, kulikuwa na upendo wa aina yake, sijui niseme nini.

Vijiji vya jirani kama vile Ibindo, Manawa, Nyamengele, Mwamajela, Goshi, Shushi, Walla na maeneo mengine wote walijumuika katika sherehe hiyo. Baadhi yao walichangia kile walicho kuwa nacho. Waliokuwa na uwenzo wa nafaka walifika na nafaka zao, walio kuwa na mifugo, nao pia walifika, mwenye mbuzi mmoja, wawili na hata wengine walijumuika wakiwa na ng'ombe mzima.

Kilicho wezekana kuletwa kililetwa, hadi vibanda vya muda vilijengwa kwa ajili ya hifadhi. Pombe za kienyeji ndiyo usiseme tena. Michezo mbalimbali ilifanyika. Michezo ya Bugobogobo, Buzwilili, Banunguli. Wigashe kwa vikundi vya Bagalu na Bagika vyote vilistarehesha umati wa watu.

Wakuu ama viongozi wa vikundi mbalimbali, waliokuwa wanafahamika kwa mambo ya kishirikina na kadhalika, baadhi yao walifika na kumfanyia ibada zao za kimila mtoto ambaye ni baba yangu. Pia walikabidhi vifaa mbalimbali kama Ichimu (mkuki), Buta na Masonga (Upinde na mishale). Wengine walitoa Ngao, Vigoda, Ngozi za Chui yote hayo ilikuwa ni kumhakikishia usalama wake kwa imani ya mila.

Wanavijiji walikula, walikunywa, walicheza na walilala na waliamkia yale waliyoanza nayo. Iliwachukua siku sita. Siku zote hizo walikuwa na hamu ya kusikia ni jina gani litatolewa kwa ajili ya mtoto ambaye ni baba yangu. Hadi siku ya saba, ambayo ilikuwa ni siku ya mwisho ndipo jina likatajwa rasimi kuwa ni "MABINA" ambalo lilidumu kwa umaarufu mkubwa hadi mwisho wa maisha yake na bado linaendelea kudumu.

Jina hilo, lina maana ya furaha, ngoma au michezo ya kienyeji iliyoendana na mila. Hivyo basi wote wenye jina hili MABINA kila mmoja ana historia yake tofauti na hii yangu.



(2)


Nyambiti ilivyokuwa:-

Yale niliyoyakuta hapo Nyambiti, wengine mtasema au mtauliza nilikuwa natokea wapi? Jibu ni zuri tu. Ni safari ya miezi isiyopungua tisa tumboni mwa mama yangu hadi nilipoiona Dunia. Pia na muda wa makuzi yangu ya kuufikia umri wa  ufahamu wa kuelewa pamoja na kuhifadhi kumbukumbu.

Kabla sijaendelea, kwanza ebu nijaribu kusimulia yale ambayo mama yangu mzazi alipo jifungua mtoto, ambaye ni mimi nwenyewe. Nilikuwa napenda sana wakati mama yangu anapoingia jikoni kupika. Mimi nilikuwa sikosi kuwa ubavuni mwake. Nilikuwa namsumbua sana kwa maswali kadhaa wa kadha. Siku moja aliniambia kuwa ni bora alinizaa, kwani kaondoa maradhi tumboni mwake. Nilimuuliza kwa nini anasema hivyo. Badala ya kunipa jibu yeye, badala yake alimsukumia bibi yangu mzaa yeye mama. Sikuona shida, kesho yake asubuhi tu nilikuwa tayari nimeishafika kwa bibi. Kwani kutoka nyumbani kwa baba, hadi kwake ilikuwa kama mita mia mbili au tatu hivi na tulikuwa mtaa mmoja. 

Nilimkuta bibi aliye fahamika kwa jina la NG'WANA MBARUKU jina halisi ni SALMA alikuwa anahangaika na ukili wa mkeka wake. Kisha nilikaa kitako baada ya kumsalimia. Aliniuliza mbona asubuhi vile kuna nini? Nilimjibu bibi kuwa hakuna kitu ila nina swali la kumuuliza. Alitaka kujua ni swali gani hilo. Nilimwambia bibi kama alivyoniambia mama. 

Bibi alishangaa kiasi fulani, mara aliweka ukili wake pembeni kisha alianza kunipa stori. alisema hivi:- Mama aliponizaa, alishindwa kunipa ziwa yaani kuninyonyesha, kwanza hakuamini kabisa kuwa mimi ni binadamu. Mwili wangu wote uligubikwa na vinyweleo mithili ya manyoya ya mnyama, uso mzima ulikuwa hauonekani, kucha za viganjani na nyayoni vya zilikuwa ni ndefu isivyo kawaida. Pia nilikuwa na mkia mfupi sana. Hivyo mama aliniogopa. Wakati wa kuninyonyesha  alibidi ajifunike nguo usoni ili asiweze kushuhudia nilivyo.  Bibi alikuwa karibu sana na mimi. Alifanya hivyo hadi hapo hali ilipokuwa inabadirika taratibu, kutoka hatua fulani kwenda hatua nyingine iliyomdhihirisha kuwa mimi ni binadamu, wala sivyo alivyonichukulia mama yangu kuwa mimi ni myama, tena ni mnyama simba.

Wakati wote bibi alipokuwa ananisimulia, sikuchoka kujiangalia mikononi, miguuni na kifuani. Mara nilikuwa najifunua shati najiangali tumbo kifua nakadhalika ili kuhakiki iwapo ile hali nilikuwa nasimuliwa je, badi ipo? Lakini wakati huo ilikuwa imekwisha. Ila bibi aliniambia nikachukue kioo ndani. Nilipo mletea aliniambia nijiangalie usoni halafu nimwangalie na yeye. Baadae aliniuliza  kuwa, je, sioni tofauti iliyopo kati yake na mimi? 

Nilijiangalia sana lakini sikuweza kubaini alichomaanisha. Alipoona nimeshindwa kubaini, aliniambia niangalie nywele zangu zimeanzia na zimeishia wapi. Nilijikuta namwangalia bibi mara mbili mbili. Niligundua kuwa, nywele zangu zimeanzia karibu sana na nyusi, na zilimalizikia usawa wa mabega. Lakini bibi aliniambia, hali hiyo  itakwisha taratibu.

Nilirudi nyumbani, nikamueleza mama bibi alivyonisimulia. Lakini mama alifanya kama kunikalipia kwa maneno kuwa, "Basi inatosha nisimkumbushe. Niliamua kuondoka nikaenda zangu kucheza.

Sasa turudi Nyambiti yetu nilivyoikuta,, wakati huo ilikuwa ni nzuri. Mandhali ya Nyambiti ilikuwa inapendeza kwa kweli kuliko hata Ngudu, Malya, Malampaka, Mantale, Magu, Misingwi na kwengineko. Nathubutu kusema hivyo kwa sababu. Kwa wakati huo palikuwa kama kituo cha kitalii. Wenyeji waliokuwa karibu na Nyambiti na sio wa vitongojini tu, bali hata wale walikuwa kwenye himaya za miji mingine, walifunga safari kwenda Nyambiti kufanya makusudio yao waliyokusudia.

Iwe ni mchezo wa mpira wa miguu, kwa lugha nyingine "football", mpira wa mikono "volleyball," ulikuwa ni maarufu kwa wenzetu Wahindi, Nyambiti ilikuwa mahali pake.

Kulikuwa na muziki wa dansi, lelemama, ngoma za kienyeji, Bugobogobo, Buzwilili, Bununguli. Makundi mbalimbali ya michezo ya mazingaombwe na mingine mingi tu.

Barabara kuu zilikuwa mbili tu, itokayo Malya kupitia Nyamiselya Goroma hadi Mantale. Iliyoungana na Usagara hadi Kisasa na kuingia mjini Mwanza. Barabara ya pili ilikuwa inatoka mwanzo wa mji hadi mwisho wa mji. Barabara hii ilitokea alipokuwa Ng'wana Shagembe alinyoosha hadi kwa Ng'wana Kishosha na kuungana na barabara ya kwanza. Pamoja zilikuwa ni za vumbi lakini zilikuwa na uimara wake uliokidhi mahitaji, zilikuwa na mifereji ya kupitishia maji, daima zilikuwa zinafanyiwa usafi.

Barabara za mchepuo zilikuwapo, moja ilitoka ulipo kuwa msikiti wa Wahindi  JAMATINI au jirani na lilipo kuwa  DUKA YA FURAHA au  ROSHNALLI kwa sasa ni miliki ya familia ya SHIJA YUSUF jina maarufu MASOLWA. Lakini alikuwa na jina la mtaani alikuwa anaitwa MWAMERIKA. Wengine mtaniuliza ama mtaniuliza kwa nini huyu ROSHNALLI aliitwa DUKA LA FURAHA? Mzee wetu nae aliitwa MWAMERIKA

Mchepuo huo wa barabara ulipitia kwa mzee wetu "Aljabril" kuelekea relini hadi shule ya Tallo na kundelea. 

Mchepuo mwingine kwa bibi yetu MAARWA. Huo ulienda moja kwa moja hadi darajani Mwamajela. Uliungana na na barabara kuu iendayo Ngudu.

Mchepuo mwingine ulikuwepo hatua chache kutoka kwa Ng'wana Kapama, aliyekuwa hakimu Mahaka ya Mwanzo. Mchepuo huo ulikuwa unapitia maeneo karibu na bwawa lililokuwa linaitwa ILAMBO LYA KUG,WA NZUNGU. Uliendelea hadi kituo cha Train Bukwimba Nkalalo.

Kiuchumi na huduma za kijamii, kwa wakati huo zilionekana kutokuwa na kasoro. Sikuwahi hata siku moja kusikia manung'uniko. Kulikuwa na wafanya biashara mbalimbali walijihusisha na biashara za nafaka, mavazi, na mazao nakadhalika.

Barabara kuu ilikuwa imepambika kwa wafanya biashara hao. Nilimtaja ROSHANALLI. Biashara kuu kwake ilikuwa nguo.

Vilevile kulikuwa na mwingine wenyeji walimpa jina la "Kalikali", nae pia akijihusisha na biashara ya nguo. 

Alikuwepo "Mamudalli" na C.K.Patel biashara zao zilikuwa kama wengine. Lakini walikuwa na vituo vya mafuta ya Petroli, Dizeli na mafuta ya taa.

Mwingine alikuwa Jaffer alijihusisha na biashara ya kununua ngozi za ng'ombe, mbuzi na kondoo. Pia alikuwa na kituo cha mafuta kama wengine.

Mwingine alikuwa ni aliyepewa jina la jina Jeremani, huyu nae  biashara kuu ilikuwa ni hizo Ngozi za ng'ombe, mbuzi na Kondoo pamoja katani au mkonge uliokobolewa "Bunella."

Hali kadhalika alikuwepo walimpa jina la "Kipala". Vilevile mtoto wa C.K.Patel alikuwa anaitwa Jent, pamoja na aliyeitwa Nkwelema, huyu alioa binti wa C.K.Patel. alikuwepo D. K.Patel ambaye ni mdogo wa C.K.Patel.

Baadhi yao walikuwa na mashine za kukoboa na kusaga nafaka, wakati wa usiku mashine hizo zilitumika kufua umeme. Nyambiti ilikuwa Nyambiti, palifanana na mitaa ya miji ya mikoa iliyokuwa na umeme wa kitaifa.

Mbali na hao, walikuwepo wenyeji ambao nao walijaliwa kuwa mali kwa biashara walizokuwa nazo.  Bwana Khasim Nyanda Mgata alikuwa ni mmojawapo, alikuwa na mshine ya kukoboa na kusaga nafaka, pia alikuwa na maduka ya bidhaa mbalimbali, Sehemu ya vinywaji vikali na baridi yaani Bar. Pamoja na biashara ya kununua nafaka yaani mpunga na ununuzi wa ngozi za ng'ombe, mbuzi na kondoo.

Alikuwepo Jirephano Mabawa na alikuwa na mdogo wake Marko Mabawa walikuwa na mbiashara hizo mbali na useremala aliokuwa nao Marco Mabawa, ambaye alihamia Nyashana baadaye alipewa madaraka ya ubunge na kisha kuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga.

Walikuwepo wengi sio rahisi kuwakumbuka wote kama vile Ng'wana Mpunganya mkubwa na mdogo, pia Hussein Bachu.

Nyambiti ilikuwa na huduma za kijamii. Kila nyumba waliokuwa na uwezo waliweka bomba za maji. Bwawa kubwa lilijengwa ambalo lilihudumia wenyeji pamoja mifugo. Enzi hizo waliliita Nyanza. Sehemu maalum zilijengwa kwa ajili ya huduma za wanyama yaani mifugo. Hata visima vya chini vya kupampu vilichimbwa katika baadhi ya maeneo ya Nyambiti.

Kituo cha afya, elimu na Mahakama vilikuwepo Ibindo. Kwa namna moja au nyingine wananchi walipaswa kuzifuata huduma hizo masafa marefu. Kituo kingine kilikuwa huko Iseni ambako kulikuwa nawakunga, ila kilikuwa chini ya umiliki wa Romani Katoliki.

Hivyo hapakuwepo na vituo vya huduma hapo Nyambiti, bali kulikuwa na kituo kimoja tu cha Elimu kwa ajili ya wenzetu wenye asili ya Kiasia (Wahindi). Kituo hicho kilikuwa kilipo sasa kituo cha Polisi na Mahakama.

Usafiri wa kwenda mjini Mwanza ulikuwepo, ingawa wakati huo barabara zetu zilikuwa ni za vumbi. Kampuni moja ya Tanganyika Bus Service iliyokuwa chini ya miliki ya Masingasinga (Singhs) ndiyo iliyo husika katika usafiri.

Ukweli enzi zetu hizo, ilikuwa ni raha tupu. Nilitegemea sana hali hiyo ingeweza kukuwa na kupanuka zaidi. Lakini mategemeo yangu yalikuwa sivyo. Nyambiti ilianza kidogo kidogo kufifia na mwisho ilipoteza umaarufu wake na hasa katika muonekano mzima wa sifa nilizo zitaja.

Ilinipa shida sana kutambua ni kwa nini imetokea hivyo. Ila fikra zangu zilinipeleka kwenye sifa moja ambayo sikuitaja, ambayo ni mambo ya kishirikina. Kuna kwani waliogopewa sana. baadhi ya wenyeji waliosifika katika mambo ya ushirikina. Nyambiti ilikuwa na sifa ya 'UCHAWI'. 

Nathubutu kusema hivyo, kwani niliwahi kushuhudia mimi mwenyewe, sikuamini macho yangu. Kwani kila ilipokuwa inatimia saa moja ya jioni, mambo yalikuwa siyo mambo. Kundi la Fisi walikuwa wakifukuzana kutoka kwenye vipenyu vya nyumba za wenyeji, lakini cha ajabu fisi hao walikuwa wamevishwa mishipi kwa maana ya mkanda shingoni mwao pamoja na kengere maarufu kilugha Ng'hinda. 

Kwa utundu niliokuwa nao, siku moja liliniijia wazo la kuwakamata fisi au Mboto hao mmoja baada ya mwingine. Nilifanikiwa kumnasa katika mtego niliouandaa mimi mwenyewe. Lakini katika harakati za fisi huyo kujiokoa alikufa. Mwenye fisi huyo alipofika kwenye tukio alilalamika sana na kisha aliuliza ni nani kafanya hivyo. Kipindi hicho maendeleo niliyo yataja yalikuwa bado, hata shule nilikuwa badi sijaanza.

Baadhi yenu watapenda kujua ni jinsi au utaalamu gani niliutumia kumnasa fisi huyo. Ulikuwa ni mtego wa kawaida tu. Enzi hizo kulikuwa kitu kinaitwa Debe hizi debe walikuwa wanafungashia bidhaa kama vile, mafuta ya kula, peremende nakadhalika. 

Nilimshirikisha mpwa wangu Mussa Mrisho mtoto wa dada yangu mkubwa, tulichukua debe lililo kuwa na tundu kiasi cha kuingiza kichwa cha mbuzi kisha, tuliweka kiasi fulani ya mabaki ya mifupa ya ng'ombe ndani ya debe hilo na kisha kuitegeshea kwenye vipenyu vya fisi hao.

Muda wao ulipo fika fisi kama kawaida ya yao walianza kujitokeza kutoka kwenye vipenyu vyao. Fisi huyo katika nusa nusa yake aligundua kuwa kapata mulo. Ilibidi alazimishe kuingiza kichwa chake kwenye hilo debe. Baadae ilikuwa hawezi tena kukitoa kichwa chake. Tulichofanya ni kumchapa viboko. Kutokana na mchapo huo, alikuwa anakimbia ovyo asijue alikokuwa anakwenda. Matokeo yake alikuwa anajibamiza kwenye kuta za majengo na mwishowe alikufa.

Wakati nimeisha anza shule, pale nyumbani kulikuwa na uuwanja au ugo kwa lugha nyingine "Fance", iliyojengwa kwa fito za miti na mmea fulani maarufu "Madete au mabengo bengo. Muziki wa dansi na naina zingine za muziki zilikuwa zinafanyika hapo nyumbani. Kilicho nitoa jasho, siku hiyo hapakuwa na shughuli yoyote ya kimziki. Baba aliwasha taa aina ya karabai akiweka uwanjani, pia alifungua chombo cha mziki aina ya " Gramaphone.  

Wale wa enzi zile wanafahamu kilikuwa ni chombo cha aina gani. Muziki ulipoanza kuchezeshwa, alitokea paka aliyeruka kutoka  nje. Paka huyo alianza kucheza muziki aina ya"Twist" kwa miguu yake miwili ya nyuma, huku akiwa amesimama wima kama binadamu.

Kulikuwa na tukio jingine, wachawi waliingia  chumbani usiku kwa minajili ya kumchukua mdogo wangu wa kike. Lakini siku hiyo iliamriwa mimi na mdogo wangu wa kiume nikalale katika hicho chumba. Naye mama mdogo pamoja na mwanaye huyo wa kike ambaye alikuwa mgonjwa, walihamia kwa bibi Ng'wana Mbaruku mzaa mama zangu.

Wachawi hao ambao walikuwa watatu, mzee mmoja, wawili walikuwa bado vijana, wote niliwatambua hata kwa majina yao. Walivyoingia waliweza kuoneshana mahali nilipo na mdogo wangu tumelala kitandani, wakiamini kabisa ni yule mgonjwa na mama yake yaani huyo mdogo wangu wa kike. Alianza wa kwanza kunifuata kitandani. Lakini hakufanikiwa kutuona. Alifuatia mwingine naye halikadhalika mambo yalikuwa yaleyale. Mwisho alifuata yule mzee, tena akiwatolea vijana wake kwamba ni wapuuzi. Lakini naye pia alirudi kwa unyonge. Nilimsikia anawaambia kuwa "kwa leo tumeshindwa tutarudi siku nyingine."

Tukio jingine lilikuwa wakati nimeisha anza kazi, wachawi walifungua dirisha langu usiku nimelala, walikuwa wawili nao niliwatambua mmoja baada ya mwingine, wote walikuwa wanawake wa makamo. Hawakunisemesha chochote bali walinicheka tu. 

Wengine nao waliwahi kunifukuza usiku nilikuwa natoka nyumbani kwa mama mkubwa. Kwa ghafla niliona vivuli vya maumbile ya binadamu wenye mavazi mieusi. Ilisikika sauti ya mmoja wao anawaamuru wenzake wanikamate kwa kuwa nimekanyaga vyungu vyao na kuvivunja. Hata hivyo niliwahi kuingia dani, nao waliishia kusema kuwa "eti nina bahati wangenishika ningejuta kuzaliwa, eti ipo siku watanishitukiza tu, kwa sababu najifanya kumlinda baba yangu."

Mbali na yote hayo fikra  zangu hizo za uchawi, hazikuwa sahihi kabisa. Baadae nilikumbuka kauli mbiyu iliyotolewa na Baba wa Taifa Hayati Rais wa kwanza Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyokuwa ni 'Siasa ni Kilimo'. Kauli hiyo haikuchagua mtu, kila mmoja alitakiwa awe na ekari moja ya yenye mazao. Kauli hiyo ilitafsiriwa vibaya kwamba, hutakiwi kuweka msaidizi wa shamba, bali ekari hiyo uihushughukie wewe mwenyewe.

Wafanya biashara hao wa Kiasia, waliamua kuondoka kuepuka zoezi hilo na wakarudi mjini Mwanza, wengine walirudi makwao India. Majumba yao yalibaki yakiwa hayana watu wa kuishi. Wengine waliyauza kwa wenyeji waliokuwa na uwezo hata baba yangu alinunua kiwanja cha Mhindi Jeremani. Hapo ndipo hata huduma zingine za kijamii zilizorota.

Kwa maana kuwa, kumbe wafanya biashara hao walikuwa wanaweka nguvu pale palipo onekana pana lega. Huduma ya maji ilikatika baada ya mshine ya kusuma maji ilipo ibiwa na watu ambao hawakutambuliwa. Nyambiti ikawa gizani totolo. Ilifikia kipindi ukisimama barabarani kwa Mzee Shija Yusufu, halafu uangalie kwa Mustafa Bugabu. Ilikuwa huwezi kuona mtu anakatisha wakati wa mchana.

Kwani hata shughuli za kibiashara zilihamia Magu na Ngudu. Ikawa Nyambiti  utadhani pamefikwa na msiba mkubwa. Palikuwa ni kimya mno. Ilifikia hata sisi wazawa tulikata tamaa, hatukutaka kuleta maendeleo yoyote kwenye eneo letu.

Kingine, ilikuwa ni uhafifu wa ulinzi, liliingia janga la ujambazi kuwavamia wafanya biashara usiku wamelala, walivunja na kuwaibia mali zao wale ambao walikuwa bado hawajaamua kuondoka. Yaliwahi kutokea hata mauaji katika harakati za kupambana na ujambazi huo.



(3)


Mabina.

Hebu tumuone huyu "Mabina". ambaye ni baba yangu. Wakati wa kupewa jina hilo, alifanyiwa mambo mengi ya kidesturi na mila. Kwa mujibu wa yale niliyo yashuhudia kwa macho yangu, baba alikuwa mpenzi wa ngoma za kienyezi na hasa zile za kucheza na nyoka kama nilivyo zielezea huko nyuma. Pamoja nilikuwa ni mdogo wakati huo, lakini nilikuwa na ufahamu wa kutambua na kutunza kumbukumbu.

Kuna mwana michezo hiyo, tulizoea kumwita Babu, kwa jina lake maalum " Nsembi". Alikuwa anapenda sana kwetu kuwa ni sehemu ya makazi yake, alipokuwa anakuja kuonesha michezo hiyo akiwa na kikundi chake. Mwingine nae alikuwa anatokea sehemu za Songwa mkoani Shinyanga. Nilimfahamu kwa jina la " SHILOLE".

Wote hao walikuwa na kawaida, kabla hawajaanza michezo yao. Walikuwa wanatukusanya sisi watoto na kutuweka sehemu maalumu, kisha anampitia kila mmoja wetu na kutushikisha nyoka. Baada ya hapo ndipo walipoweza kuendelea na maonyesho yao.

Pale nyumbani, mara kwa mara nyoka walikuwa wanaingia ndani mwetu. Lakini tunapomwambia baba, alitujibu kuwa tumwache atatoka mwenyewe. Ilikuwa ni balaa huwezi kuamini, nyoka hao walichukua muda mfupi, walitoka na kisha kutoweka. Hata hivyo alitukanya na kutuonesha ni nyoka wa aina gani tunapaswa kumuua mara tunapowahi kumuona.

Baba huyu aliwahi kuonesha maajabu, alichukua kibuyu kikubwa, akakikata mfano wa chungu. Kisha aliinjika kwenye moto viazi vitamu ndani ya kibuyu hicho. Viazi viliiva na watu wakala. Fikiria kile ni kibuyu kiliwezaje kuuvumilia moto wa kuni bila ya kuteketea?

Siyo hayo tu, bali aliweza kuwachukua watuhumiwa wa Uchawi, ambao waliwagomea viongozi wa Nyambiti kuchukuliwa kuwapeleka kwa mkuu wa Wilaya. Ugomaji wao uliambatana na gari kutofanya kazi. Lakini walipo mtaja "MABINA", mabibi wote wachawi, walishangilia na kusema kuwa, wapo tayari kupelekwa naye na wala si mwingine. Ni kweli aliwachukuwa gari lake hadi kwa mkuu wa wilaya Ngudu.

Wengi wa kila lika na hata vikundi mbalimbali walimpenda, wakati huo kulikuwa na burudisho la mchezo wa " LELEMA." hakukosa kukaribishwa, na kwa wakati mwingine aliweza kutumia chombo chochote katika burudisho hilo.

Wakina mama waliokuwa na desturi za "UNYAGO", mara nyingi walikuwa wanampa wito wa kuhudhuria. Sasa fikiria, Unyago ni kwa ajili ya jinsia ya kike tu kwa ajili ya mambo yao. Je, wana unyago walimpendea nini? Alikuwa na lipi la kufanya huko? Hakuna aliyejua, ilikuwa ni siri yake.

Hata katika uongozi wa kijiji alishika nyadhifa mbalimbali. Viongozi wa serkali kutoka wilayani na mkoani ilikuwa lazima wafikie hapo nyumbani. Nilishuhudia hata askari wa fanya fujo uone, walikuwa wanafikia kwetu. Wakati huo walikuwa wanafahamika kwa jina la " MOTORISE".

Mbali na hayo. Baba alijishughulisha pia na mambo ya biashara. Kwanza kabisa, alianza kuwa na mgahawa hapo hapo Nyambiti. Kwa muda mfupi, mimi niliondoka kwenda Musoma. Niliondoka na shangazi yangu Gwalihwa.

Shangazi yangu huyo alikuwa na maradhi ambayo aliombwa na mdogo wake kwa mama yao mdogo kwamba amchukue akamtibie huko ambako alikuwa ameolewa.  Tulipofika huko taratibu zote zilifanyika na aliendelea na matibabu.

Wakati huo umri wa kuanza shule ulikuwa umeisha timia. Mume wa shangazi mdogo alichukua jukumu la kunisajili shule. Lakini kabla ya hapo nilipelekwa kanisani kubatizwa. Tendo la ubatizo halikuwa ndani ya ufahamu wangu. Niliona kama vile mchezo fulani wa kuigiza.

Baada ya muda fulani Shangazi Mkubwa alifahamu tukio hilo ambalo halikumpendeza, aliamua kunirudisha nyumbani.

Wakati huo nilimkuta baba anashughulika na biashara ya duka bidhaa mbali mbali. Biashara hiyo aliifanyia kijiji kingine mbali na Nyambiti. Baadaye duka lilifilisika nikiwa darasa la pili shule ya msingi Walla na baadae nikahamia shule ya msingi Shushi. Maendeleo ya biashara hiyo ilikuwa afuate masharti aliyopewa na mtaalamu. Lakini alishindwa kutimiza. 

Alishindwa nini kutimiza? Alipewa sharti la kumpokea mgeni, kisha amfanyie ukarimu. Sasa ilikuwaje, mgeni ni nani basi? Ilikuwa ni asubuhi anafungua mlango atoke nje. Ndipo alimkuta mbwa mkondefu, mchafu hadi tongotongo zinamtoka machoni amelaka kizingitini. Alishindwa kuvumilia na wala hakuwa na wazo lolote kihusu mtaalamu. Aliishia kumfukuza na kumpiga mateke. Kitendo hicho utajiri alifukuza. Yule mbwa ndio alikuwa mgeni.

Mwisho aliamua kuwa mkulima eneo moja linaitwa Talaga. Kipindi hicho nilikuwa darasa la nne. Utajiri wake ulitokana na Kilimo. Kwani ilikuwaje, ilikuwa hivi:

Baada ya kufirisika alirudi kwa mtaalamu aliyefahamika kwa jina la Buyugu huko Ntuzu, ambaye alikuwa ni mtaalam wa kuwapatia watu utajiri. Baada ya kuwa alifanya makosa katika masharti ya awali, alipewa nafasi nyingine ambayo ilikuwa ni ya kilimo.

Katika harakati za maisha, alitokea kuwa fundi mzuri wa mtambo wa kushusha na kupandisha majembe ya trakta. Kila trakta lililo letwa kwake utafiti ulikuwa anaufanya shambani, ilikuwa analima nusu ama ekari nzima. Alifanikiwa kumaliza kulima shamba lenye ekari kumi kwa mtindo huo. Ekari zote alizipanda pamba. Pamba ilimea vizuri sana, hadi ilipofikia kiwango cha kuweka maua, lilitikea tukio la ajabu.

Ilitokea mvua iliyoambatana na mawe, ilivunja vunja mimea yote, kiasi ambachio kilimkatisha matumaini. Alizila kufika shambani kwa uchungu. Bila mategemeo alikuja mwana kijiji wa huko aliko limia shamba hilo. Alimwambia mimea ya pamba ipo kwenye nyasi, hivyo alimtaka akaifanyie palizi.

Lakini hakutaka kuamini maneno ya huyo mwana kijiji. Mke wake ambaye ni mama yangu, alifunga safari hadi shambani. Mama alishuhudia taarifa ya yule mwana kijiji kuwa yalikuwa ni kweli. Taarifa alimfikishia baba.

Siku iliyo fuata baba alishuhudia kwa mshangao mkubwa, kweli Mungu acha aitwe Mungu. Pamba ilikuwa nimestawi kuliko kawaida. Hakutaka kupoteza muda, alifanya mwaliko wa wana kijiji wamsaidie kuilimia palizi. Ndani ya siku nne, ekari zote kumi zilikwisha. Kweli zama za wakati huo, kulikuwa na ujamaa na upendo. Gharama yao kubwa ilikuwa ni kupikiwa chakula na kinywaji cha pombe ya kienyeji Kangara au Swezo.

Pamba iliendelea vizuri hadi ilipofika wkati wa kuvunwa. Halikadhalika ilivunwa na wana kijiji. Pia wakati wa mauzo, ilibidi wakulima wengine wasitishwe kwa siku tatu nzima. Malipo ya zao hilo ilibidi akalipwe makao makuu ya mkoa Mwanza. Kiasi alicho pata hakuna aliyejua, labda mama sina uhakika.

Hapo ndipo akaibuka kununua magari. Alianza na gari Peogeut Pick Up moja, baadae akanunua Land Cruiser moja, Bedford Lorry mbili, Mercedes Benz Lorry tatu, Tractor moja na Hiace moja. Aliendelea na ufundi magari, hata hivyo asilimia kubwa alikuwa anatengeneza magari yake mwenyewe. Kilimo kwake ikawa kama ibada. Hayo ndiyo mafanikio aliyo yapata niliyo yashuhudia mimi mwanae.


"Sura ya Pili"

Mwanzo wa elimu:

Madrasa 

Maisha ni safari, hii ni kweli haina pingamizi. Katika harakati ya safari yangu hiyo, elimu ilikuwa ndilo jambo la msingi walilo kuwa nalo wazazi wangu haw wawili.

Nilianza na elimu ya dini..kwa.imani yangu na familia. Nina maana ya Chuo au Madrasa.Madrasa ilikuwa ni jirani tu na nyumbani, ilikuwa ni nyumba ya tatu kutoka kwetu. Nakumbuka mmliki wa eneo hilo la Madrasaalikuwa ni Bwana Idd Baruti.

Idd Barti alikuwa na familia yake akiwemo Juma Idd Mshilimu, Ng'wana Nduta na wengine.

Ng'wana Salomu, alikuwa jirani kwa upande wa kulia, mwanae aliolewa na mzee Idd Baruti, wakamzaa mtoto waliye mwita Khadija.

Watoto tulikuwa wengi hapo madrasa, baadhi nawakumbukaakina Kheri Hussei Karuta, Hassan Ali Timami, IbrahimuAbdallah Kabhi, na wengine wengi waliokuwa wametuzidi umri kama vile Idd Mzee,Omari Mzee, Salehe Husseinna Mjahidi Hussein. Mwalimu wetu alikuwa maalimu Hussein Karutta.

Lakini utoto ni utoto tu. Mahali pangu nilipokuwa napendelea kukaa ilikuwa ni jirani na dirisha. Kwa nini? Kwa sababu yule maalim Hussein alikuwa anatembeza viboko ile mbaya. Akianza kuchapa hachagui nani mkosaji na wapi pa kuchapa. Kaa yangu jirani na dirisha ilikuwa mara kichapo kilipo kuwa kinaanza,basi mimi nilikuwa nawahi kuruka na kutoka nje.

Walikuwepo mashekhe na wazee wengine waliokuwa maarufu kwa uzee wao na taaluma zao pia. Namkumbuka shekhe Maalim Shaaban alikuwa anaishi jirani na shekhe Maalim Said na kwa Ng'ambo ya barabara walikuwepo mzee Mabawa na Mzee Ramadhan Kitambi (Ngalu).

Shule ya Msingi.

"Ukizu".

Wakati nipo Musoma kwa minajili ya kumsaidia Shangazi aliyekuwa ni mgonjwa. Nilisajiliwa kuanza shule kama nilivyo elezea huko nyuma. Nilianza darasa la kwanza katika shule ya msingi Ukizu ikiwa katika miliki ya shirika la dini ya Kikristo "Sabato". 

Shangazi mdogo alikuwa na mwanae wa kiume ambaye tulikuwa lika moja na shule tulianza pamoja. Baba yake alimtaka kimapenzi Shangazi yangu mkubwa,ilipo shindikana alitumia njia mbadala ya kumvizia usiku amelala, nayo ilishindikana na alijikuta akiwa ni mtu wa aibu kwenye jamii. Ulifanyika uchokozi fulani ili nipigane na mtoto mwenzangu. Matokeo yake nilimjeruhi karibu na jicho kiasi kilicho pelekea mimi kuwindwa ili niuawe kwa kuchomwa mshale. Hali hiyo ilijitokeza muda wa jioni ambapo nilikoswa koswa mshale uliokita kwenye shina la mti. Shangazi aliamua tuondoke jioni hiyohiyo, tulilala kwa kiongozi wa kitongoji. Asubuhi yake tulielekea kwa mtaalamu.

Shangazi alipo nirudisha nyumbani kutokana na mambo yaliyotokea, baba alinieleza kijiji cha Walla ambako kulikuwa na shule ya msingi. Ni moja kwa moja nilianza darasa la pili badala ya darasa la kwanza, kwani nilionekana nina upeo wa juu kuliko niliowakuta wakiwa darasa la kwanza.

Shule ya msingi Walla:

Nilikabidhiwa kwa mwalimu mmoja namkumbuka kwa jina moja tu alikuwa anaitwa Mohamed. Niliishi kwake kwa muda wote niliokuwa hapo. Mwalimu huyu hakuwa na mke alikuwa single kama msemo wa wengine. Kutokana na hali hiyo ya mwalimu huyo, mimi nilikuwa ndiyo mtendaji mkuu wa nyumbani. Mambo ya usafi ndani na nje ulikuwa mikononi mwangu. Ilibidi niamke asubuhi na mapema ya alfajiri kukabiliana na shughuli hizo. Mbali na hilo kazi ya shamba ilikuwa ni wakati wa jioni nilipaswa kwenda. Hizo ni baadhi tu ya shughuli nilizo kuwa nazifanya. Lakini zilikuwepo nyingi nyingi sana nje ya uwezo wangu. Sikuwa na jinsi ilibidi kuzifanya. Hata hivyo utoto nao ulinisaidia, pamoja niliona Kama ni uonezi na unyanyasaji, haikuchukua mwingi wa kusononeka.

Hapo shuleni Walla palikuwa na walimu wawili tu, na enzi hizo palikuwa hakuna habari ya mkondo A au B. Darasa moja lilitakiwa kuwa na wanafunzi arobaini na tano tu. Hivyo basi wakati mwingine idadi hiyo ilikuwa haitimii.

Shule zilikuwa chache na hata wanafunzi walikuwa wachache, vile vile idadi ya watu nchini ilikuwa ndogo sana. Wakati huo bila shaka idadi ya watu inchini ilikuwa ni milioni saba na kidogo. Lakini leo hii ni maradufu

Hebu nirudi nyuma hapo Nyambiti. Alikuwepo mzee wetu Mashamba mkubwa na mdogo. Mkubwa alikuwa anaishi Nyambiti Ginnery kama sikosei. Hapo palikuwa na kiwanda cha kuchambulia pamba. Huyu mdogo alikuwa jirani na nyumba yetu. Yeye alikuwa Ng'ambo ya barabara na alikuwa mkorofi sana. Kuna siku alikwaruzana na Bw Ally Kishosha, alimpiga na rungu akazimia, tena ilikuwa ni pale pale nyumbani alipo mbele ya fundi cherehani alipo mzee Rashidi Mnyiramba (Kukokotwa).

Mtaa wa nyuma wa nyumba yetu alikuwako mzee Ismail Kinongu. Mzee huyu alikuwa anatembea na bakora. Alikuwa na sifa ya mzee mwenye nguvu, akikushika huwezie kujitoa. Pili alikuwa anakula siyo kawaida. Tonge yake moja ni sawa na tonge tatu kwa mtu wa kawaida. Hata kwenye sherehe alikuwa anapewa chakula chake peke yake.

Vilevile alikuwapo mzee Ramadhan Kilemba. Huyu alikuwa maarufu kwa jina la makoroboi, kwani alikuwa fundi wa kuunda taa za tambi maarufu koroboi. Pia alikuwepo mzee Shadi ambaye alikuwa kiongozi wa kitongoji na kisha akamuachia kijiti Ali Kishosha. 

Mwingine ni mzee wetu Iddi Kija. Tulimpenda sana kwani alikuwa mtetezi wetu vijana tuliokuwa tunachukulia. Alikuwa hapendi maonezi alikuwa tayari kupigana na mtu yeyote yule kuitetea haki yetu.

Kaka yake mzee Hamza Kija alikuwa fundi cherehani, alikuwa mtu mpole sana asiye taka makuu. Baadaye alipata madaraka kwenye chama cha TANU kwa ni CCM.

Mabula Bukonze, naye pia tulimpenda kwa sababu alikuwa anatuweka kuwa imara. Alikuwa anatupa mazoezi ya kupigana kwa ngumi, ila alikuwa anaogopewa sana na jamii.

Ilikuwa inafurahisha sana tulipokuwa tunaenda kucheza mpira na timu za Ngudu, Malya, Misingwi au Magu. Furaha yetu ilikuwa tunajisikia tupo huru wakati wanapo jumuika hao niliowataja pamoja na Mahamoud Khabhi na wengineo. Hata ikitokea fujo ya jinsi gani walikuwa wanaimudu kwa mapambano.

Ilitokea timu ya Nyambiti kuingia fainali na timu ya Misingwi. Timu ya Nyambiti ilipo ingia uwanjani ilidharaulika na kuonekana itafungwa magoli mengi. Kwa nini? Kwa sababu wachezaji wa mbele na pembeni tulikuwa ni sisi vijana wadogo bado tungali tunasoma shule ya msingi. Baadhi yetu tulikuwa Ibrahim Khabhi (Kasaja), alikuwa golini msaidizi, ila kaka yake Yombo ndiye alicheza siku hiyo. Alisifika kwa mipira ya juu alivyo kuwa anaidaka, wakamwita Nyani. Wengine ni Seleman Aroni, Justo Ndaki, Bw.Kheri Hussein Kaluta, Juma Mngatta, mwamuzi alikuwa Jumanne Mandago. Kabla ya nusu ya kwanza tulikuwa tumeisha wafunga magoli matatu kwa sifuri. Kipindi cha pili tuliongeza goli la nne. Hapo ukazuka ugomvi kwamba refa anatubeba. Wababe wetu nilio wataja huko nyuma, walivamia mahali lilipo Kombe wakazuia lisichukuliwe hadi maamuzi sahihi yapatikane. Lakini kwa ufupi kombe tulilichukua.

Sasa tuendelee na sehemu yetu ambayo ni shule ya msingi Walla. Mwalimu mkuu alikuwa ni MATUZYA alikuwa mwenyeji wa mkoa wa Tabora, alikuwa na familia ya watoto watatu, wawili wa kiume na mmoja wa kike kwa wakati huo. Walikuwa wanafahamika kwa majina ya Enos, Mathias na Grace, tuliishi nao vizuri.

Mimi nilikuwa kwa mwalimu Mohamed mwenyeji wa mkoa wa Lindi. Sikujua ni kwa nini nilipelekwa kote huko, wakati kulikuwa na shule ya msingi ya Ibindo au Walla ambako baba alikuwa na biashara zake. baadaye nilibaini kuwa mwalimu huyo aliweka nia ya kumuoa dada yangu mkubwa. Lakini ilishindikana kwa sababu ya fikra potofu za makabila ya kusini kwamba baadhi yao wana roho za kinyama, kwani wapo tayari hata kukutumia kama kitoweo ambapo haikuwa sahihi.

Mwalimu huyo alitokea kuwa mlevi sana na alimpata mwanamke ambaye alikuwa anamleta pale nyumbani.

Hata hivyo alikuwa hafanyi chochote zaidi alikuwa analala na kesho yake asubuhi anaondoka. Pamoja na hayo siku wakiwa pale nyumbani walikuwa wanakunywa kilevi cha aina ya bia huku muziki wa Gramaphon ukichezwa nao pia waliinuka na kucheza.

Ilifika wakati nilimuomba baba kuhama na hasa pale shangazi yangu Gwalihwa alipotutaka sisi watoto tuonane naye akiwa ni mgonjwa mahututi. Siku hiyo alikuja baba shuleni Walla aliambatana na kaka bwana ABDALLAH MWALABU, walikuja na gari ya muhindi tuliyezoea kumwita Kipala. Nilifika nyumbani niliwakuta wenzangu wote wapo. Nilimkuta shangazi taabani kitandani, nilimsalimia na kisha alinipa maneno kadhaa kama angalizo katika maisha yangu.

Kwanza alinisihi niwe mvumilivu katika safari yangu ya maisha. alinisisitiza kutokuwa na hasira hata kama nitachukizwa kiasi gani. Kisha alimalizia kwamba mafanikio nitayapata, nitapewa heshima na nitakuwa kiongozi na mshauri ndani na nje ya familia. Shangazi aliondoka duniani baada ya siku mbili za kuongea nae.

Shule ya msingi Shushi.

Mahali tulipokuwa nyumba yetu hapo Shushi, ilikuwa karibu na bwawa lililokuwa na miamba. Ng'ambo ya barabara kulikuwa na ofisi ya Nyanza kwa ajili ya ununuzi wa zao la pamba. Mbele yake kulikuwa na maghala ya kuhifadhi zao hilo. Jirani yetu alikuwa ni mhasibu wazazi wake walikuwa wakiishi huko Solwe alikuwa na jina la Peter. Wakiwepo wengine kama Samsoni ambaye alikuwa Karani, Ng'wana Nungwana, Ng'wana Ngalaba aliyekuwa na watoto baadhi yao nilisoma nao kama vile Mary nilisoma nae hapo kisha kuna Senema nilimkuta Kinango.

Hapo shuleni Shushi nilipelekwa darasa la tatu kwani huko Walla nilikuwa nimemaliza darasa la pili. Sikuchukua muda nikahamishiwa darasa la nne, kwa maana nyingine darasa la kwanza na la tatu sikuyamaliza.

Wakati naendelea na masomo karibu ya mtihani wa kumaliza darasa nne kufanyika, nilipata maradhi ambayo nilishindwa kuyabaini. Nilikuwa si wakutoka nje takribani wiki mbili. Kitanda na mimi, mauzauza yasiyo na majibu yalitawala kwenye maradhi yangu. Siku ya mtihani ilipofika. Mwalimu alituma wanafunzi kuja kunichukua kwa baiskeli.

Lakini maajabu ni kuwa, nilipofikishwa shuleni nimekaa kwenye dawati langu ugonjwa ilitoweka. Nilifanya mtihani wangu na kisha nikarudishwa nyumbani. Matokeo yalipotokea nilichaguliwa kwenda shule ya bweni Kinango iliyoko Magu, enzi hizo ni MIDDLE SCHOOLS.

Matokeo hayo yaliwastaajabisha wengi siyo kwenye familia tu, bali hata nje ya familia yetu. 

Shushi kwa muonekano mwingine tulikuwa na bahati ya kupendwa na wenyeji. Mahali tulipokuwa tunaishi palikuwa na vurugu za hawa wanyama yaani fisi. Wakati jua lilipokuwa linapoteza nuru yake yaani jioni, basi fisi nao walikuwa wanajikusanya kwenye miamba karibu na bwawa lililokuwa jirani na nyumba yetu. Waliweza hata kufika pembeni mwa eneo ambalo tulizungushia minyaa kama Uzio. Kwani wenyeji nao walikuwa wanahoji iwapo tutastahimili kuishi hapo. Ila baba alinikanya nisije nikafaya kama nilivyo watega huko Nyambiti.

Pamoja na hayo vijana kutoka Nyambiti walikuwa wanatutembelea na hasa nyakati za jioni. Muda ulipokuwa unatimia kwa fisi hao kujikusanya basi hao vijana walikuwa wanawafukuza kwa baiskeli zao zilizokuwa na taa pia walitumia tochi zao huku wakiwachapa kwa viboko. Kama kweli kulikuwa na dhana ya ushirikina basi vijana hao wangeshirika lakini hakutokea. Vijana hao baadhi yao ni Athumani Idd Lyalika, na mdogo wake Sadiki Idd Lyalika, Jumanne Mandago,Fyetuka Nguluchape, Juma Mshilimu, Jumanne Makelemo, Omar Mzee, Abdallah Shunulla, na wengineo wengi. Fisi hao hawakuacha tabia yao pamoja na kwamba idadi yao walipungua kiasi fulani. Hata hivyo waliendelea na uharibifu wao wa kuuwa mifugo na hasa ng'ombe, mbuzi, kondoo na punda.

Nikirudi nyuma kuhusu fisi hao, siyo tu maeneo yetu ya Nyambiti na Shushi ndizo zilikuwa zinaogofya kwa wingi wa fisi hao. Yalikuwepo maeneo mengi tu ambayo fisi walikuwa ni tishio. Siku moja niliondoka na baba nikaenda naye Magu. Wakati wa kurudi nyumbani ilikuwa ni usiku, tulipofika maeneo ya Ng'waging'hi. Mara zilisikika sauti za fisi hao moja baada ya mwingine katika pembe zote nne. Baba alimulika huko na kule lakini hatuona chochote. Mara tena sauti zilisikika Kwa mbele yetu kama vile binadamu wananong,'ona, punde walianza kututisha kwa kututimulia mchanga.

Baba aliniambia nisiogope kwani dawa yao ni ndogo sana. Alichepuka upande wa kushoto, hakuchukua muda alirudi akiwa na Matango Limbe, wakati huo nilikuwa nawamulika fisi hao kwa taay baiskeli. Tuliwafuata fisi waliko. Baba aliwatupia tango moja ambalo kila mmoja wao akitaka aliguse kwa mvuto linavyoonekana kuvurugika. Baadaye aliwatupia matango yote pembeni mwa barabara, wote waliyafuata kwa kicheko sana, hivyo hawakuwa na shughuli na sisi tena. Tukapata eneo hilo bila madhara yoyote. Hivyo hapo nikawa nimepata somo.

Sio mkasa huo wa fisi tu, kuna viumbe kilugha wanaitwa KABHEBHA. Mara nyingi hutokea wakati wa usiku katika barabara au njia za kawaida. Viumbe hawa walikuwa wanaonekana kwa maumbile marefu mara mbili ya binadamu wa kawaida. Vazi lao ni nguo nyeupe toka juu hadi chini.

Siku hiyo tena tulikuwa na baba tunatoka Mantale ilikuwa ni usiku tulipofika maeneo ya Bungulwa, baba aliguna kisha aliniambia nijiangalie nyuma. Aliniambia nisiogope, lakini wakati tunageuka tena mbele ajabu nyuma na mbele yetu tayari kulikuwa na viumbe hao.

Baba kama kawaida yake aliguna tu, kisha aliniambia nisiogope, alinishikisha baiskeli ukweli niliogopa sana, lakini kwa kuwa baba alinitoa wasiwasi, nilikaza moyo.

Kwenye baiskeli ya baba kulikuwa na nyenzo asizo zisahau hata siku moja. Kwa mbele kwenye usukani kulikuwa na kisu kirefu na kikubwa kama panga ila chenyewe kilikuwa chembamba, mshiko wake ulikuwa wa mfupa wa mnyama, sijui ni wa mnyama gani? Pia kulikuwa na kiboko cha mkia wa mnyama mwenyewe kiboko. Kilikuwa kirefu sijui alikiunga vipi.

Aliniachia baiskeli, akamfuata huyo kiumbe aliyekuwa mbele yetu, hata hivyo bado nilikuwa na hofu na huyo mwingine wa nyuma yetu ingawa alikuwa mbali kidogo. Wakati huo alikuwa amejichubua kiboko chake, alijificha mgongoni ndani ya shati. Mara alipo mfikia huyo kiumbe alimcharaza kiboko kimoja tu. Cha kushangaza yule kiumbe aligawanyika mara mbili. Sehemu ya chini ilidondoka chini na sehemu ya juu alionekana ni binadamu aliyetimua mbio. Baba alicheka sana. Nilikumbuka kwamba kuna mwingine nyuma yetu, lakini nilipo geuka kumwangalia nilimuona anatokomea kwa mbali.

Baba aliniambia kuwa, huo huwa ni mchezo tu, huyo ni binadamu wa kawaida. Aliniongoza hadi mahali pa tukio, cha ajabu kile kilicho dondoka chini ilikuwa miti miwili mirefu iliyokuwa na sehemu ya kukanyagia pamoja na hayo mashuka meupe. Baba aliniambia kuwa huwa wanafanya hivyo ili kukutisha uwaone wao ni viumbe wajulikanao kama ni MAJINI. Hapo hapo aliniambia kuwa kwenye michezo ya utamaduni huwa siwaoni kama hao wakiwa juu ya hiyo miti? Nilimjibu kuwa niliisha waona. Alizidi kuniambia kuwa, basi huwa ni hao hao kwa malengo ya kuogofya na kukupokonya ulicho nacho. Ila wao huongeza kuvaa nguo nyeupe kutoka juu hadi chini kabisa. Kwa hiyo dawa yao ni kiboko tu.

Shule ya Kinango:

Siku niliyo kwenda shuleni ni baba aliyenichukua kwa baiskeli, vitu nilivyo ondoka navyo ni shuka mbili nyeupe, mto na foronya yake nyeupe, viatu ni raba nyeupe na khaki na viatu vya ngozi rangi nyeusi. Pia sikosi ndefu na fupi rangi nyeupe na khaki pamoja na sanduku la mbao.

Tulifika shuleni Kinango majira ya saa nne asubuhi. Alinikabidhi kwa walimu baada ya kulipa ada ya shule ambayo kwa wakati huo ilikuwa ni shilingi mia mbili na arobaini.

Baada ya kupokelewa nilipelekwa stoo ambako nilipewa nilipewa kitanda cha chuma aina ya Banco, godoro, blanketi, sanduku la mbao jeusi, sabuni ya kuongea aina ya lifebuoy pia na ya kufulia ya miche aina ya sunrise. Vilevile nilipewa fulana na ...... pamoja na vyombo kwa matumizi ya chakula, sahani na bakuli, kikombe, kijiko, uma, kisu na ndoo na kwanja.

Kwa upande wa darasani kuanzia madaftari kalamu aina zote tulipewa. Kudai cha wino na bibi yake kila mmoja alivikuta kwenye dawati lake, karatasi ya kukaushia wino. Kipindi hicho tulikuwa tunatumia wino wa kuchovya.

Nilipangiwa Bweni la Sensuss, wengine walipangiwa bweni la Channan, Mosses na Muya. Sensuss ilikuwa na maana ya mwaka ambao kuhesabiwa kwa watu wa Tanganyika ndipo shule hiyo ilipomalizika kujengwa. Channan ni mkandarasi aliyejenga shule hiyo, Mosses ni mtawala wa au mtemi wa eneo ilipojengwa shule hiyo na Muya alikuwa ni head masters wa kwanza katika shule hiyo.

Mazingira ya shule yalikuwa mazuri kwa wakati huo. Jengo la madarasa na ofisi za walimu kwa kusini mwake kulikuwa na uwanja mkubwa kwa ajili ya paredi nakadhalika. Kwa mbele ya uwanja huo lilifuatia jengo la chakula "Dinning Hall", lililo jumuisha sehemu ya jiko, stoo ya kuhifadhia chakula. 

Magharibi yake kulikuwa na jengo la ufundi pamoja na stoo ya kuhifadhia vifaa mbalimbali. Kwa upande huo huo pembeni yalifuatia mbweni ya Mosses na Muya. Kwa ukaribu kidogo kulikuwa na zizi la mifugo, yaani ng'ombe, mbuzi nakadhalika.

Kwa upande wa Mashariki kulikuwa na mabweni ya Channan na Census na kwa pembeni kulikuwa na nyumba za walimu pamoja na shamba la shule la mazao kadhaa.

Kwa upande wa Kaskazini kulikuwa na uwanja mdogo uliofiatiwa na Bustani ya mbogamboga, kwa mbele zaidi kulikuwa na bwawa na msitu wa shule.

Uvaaji wa sare ulikuwa ni shati na kaptula khaki pamoja na viatu vya ngozi nyekundu kwa soksi fupi za khaki. Hii ilikuwa ni kuanzia siku ya Jumatatu hadi Ijumaa. Ila siku ya jumatano tu ndiyo ilikuwa ni siku ya kuvaa viatu vya ngozi.

Siku ya jumamosi ilikuwa ni siku ya ukaguzi wa Mkuu wa shule, sare ilikuwa ni shati na kaptula nyeupe soksi ndefu nyeupe na viatu vya ngozi nyeusi, ila Jumamosi ukaguzi wa kawaida ni raba nyeupe.

Ukaguzi ulianzia usafi wa mwili, sare na kisha katika mabweni kwa kila kitanda na juu ya sanduku la shule vionekane viatu, kiwi, brashi, sabuni na mswaki na dawa yake, vyote vikiwa katika utaratibu ulio sare. Pia vitanda vikiwa katika mstari ulionyooka na mtandiko wa vitanda ni wa aina moja. Baada ya hapo ulifuatia ukaguzi wa maeneo ya nje kwani kila mmoja alikuwa na eneo lake kwa ajili ya usafi aidha kufyagia ama kufyeka nyasi na hata kukatia maua na kuyamwagilia maji. Mwisho kabisa ukaguzi uliishia sehemu ya chakula na zizi la mifugo.

Ratiba ya siku nzima ilikuwa kuanzia saa kumi alfajiri. Tuliamshwa kwa buruji. Kiongozi wa kila bweni alipeleka taarifa ya uwepo wa wagonjwa na mengineyo kwa kiongozi mkuu "Head Prefect" na kisha naye kuifikisha kwa mwalimu wa Paredi Sajenti Vicent.

Baada ya hapo tulikimbia mchakamchaka hadi zahanati ya Mwangika. Saa kumi na mbili kila mmoja alitakiwa kuwa kwenye eneo lake la usafi, saa kumi na mbili na nusu tulipaswa kuwa mess kupata uji ulio changanywa na mafuta ya mawese. Saa moja kasoro robo wote tulikuwa tayari uwajani kwa ajili ya ukaguzi tukiongozwa na Brass Band ya shule kwa uongozi wa huyo huyo mwalimu Sajenti Vicent. Ulifuatia paredi na baada ya hapo wote tuliingia madarasani ikiwa ni saa mbili kasoro robo.

Saa nne na nusu ilikuwa ni kipindi cha mapumziko pia kupata chai ya maziwa kwa mkate "Bofuro" ulio na siagi "Jimbo". Saa tano tuliendelea na masomo hadi saa sita na nusu. Kuanzia muda huo ilikuwa ni kupata chakula cha mchana iwe ugali kwa maharage au kwa nyama na mboga za majani au wali kwa samaki Sato wakati na shughuli nyingine binafsi. 

Saa nane mchana wote tulikusanyika uwanjani kwa ajili ya kugawiwa kazi za kufanya kwa ujumla. Ila siku za Jumatano wote tulijumuika katika kazi za mikono, yaani ufundi mbalimbali ambao ulikuwa na ratiba maalumu kwa wiki.

Kipindi hicho kilifanyika hadi saa kumi na moja jioni, hapo kila mmoja alikuwa huru kuendelea na mambo yake hadi hapo saa kumi na mbili wakati wa chakula cha jioni saa moja na nusu ambapo matunda Kama machungwa, ndizi karanga nakadhalika vilikuwa havikosekani. Baadae tuliingia madarasani kujisomea hadi saa nne kasoro robo wote tulitakiwa kuwa mabweni tumezima taa na kulala.

Enzi hizo majiko yalikuwa ni ya kuni na mkaa. Taa zilikuwa ni za mafuta ya taa yaani karabai na chemli. Pasi za kunyooshea nguo zilikuwa ni za mkaa pia.

Baadhi ya walimu nawakumbuka, mwalimu Shilangale, Kitimbo, Silaha, Kuzibua na Mr.Mbwana. Walimu hawa walikuwa wanafundisha masomo yote kwa madarasa yote.

Michezo mbalimbali ilikuwepo mpira wa miguu, mikono na hata riadha pia. Mwalimu wake alikuwa Padri Clement mjerumani. Alifahamika kwa la Masanja.

Nikirudi nyuma, kipindi cha likizo mojawapo nilikuwa nyumbani kwa bibi mzaa mama. Usiku niliota ndoto kwamba nimeisha kuwa mwana jeshi, nipo tayari vitani napambana na maadui. Nipo juu ya mti nikiwa na silaha yangu. Niliwashambulia adui hadi nikawamaliza wote.

Kesho yake asubuhi nilimsimulia bibi, bibi aliniambia kuwa, ndoto hiyo inanipa ujumbe kuwa siku za usoni nitakuwa askari na nitapanda cheo na kuwa afande mkubwa. Kwani huo ni urithi nauchukua kutoka kwa mababu zangu wa pande zote mbili, wote walikuwa askari wa KEYA K.A.R "King African Rifle." Wote walikuwa na cheo cha Sajenti.

Shule ya Tallo:

Baada ya miaka miwili niliamua kuhamia shule ya Tallo. Sababu iliyo nifanya kufanya hivyo ilikuwa ni kutokana na deni la ada ya mwaka wa pili. Baba alibadilika ghafla akawa hana upendo kwangu. Yote hayo yalitokana na kufarakana na mama yangu mzazi.

Mama aliondoka na kurudi kwa ndugu zake Tabora. Hapo ndipo hali ilianza kuwa ngumu kwangu, na wakati huo baba alikuwa ameleta mwanamke mwingine. Rafiki ndugu alinishauri tuhamie shule ya Tallo kuepuka gharama kubwa ya ada.

Kitendo cha kuhama kilimzidishia chuki baba yangu. Hakutaka hata kule kuniona, alinifukuza nyumbani. Maisha yangu yakawa magumu sana. Rafiki aliye nishauri kuhama, alinipa hifadhi nyumbani kwao. Baada ya siku chache baba alibaini nilipo, hakusita kunifukuza kwani ilikuwa ni jirani tu. Nitakumbukwa maneno aliyo niambia marehemu shangazi. Ila nilipiga moyo konde.

Hata hivyo nilijiuliza itakuwaje nipate ajira ya uaskari wakati hata shule sijamaliza na sijui iwapo nitamaliza kwa maisha hayo niliyokuwa nayo. Kwani ilifikia hata shule nikawa siendi kwa sababu nilitakiwa nilipe deni la ada ndipo niruhusiwe kuendelea na masomo.

Masomo ya jioni

Siku moja nilikuwa katika harakati za kutafuta riziki katika jengo la Community Centre hapo Nyambiti. Ilikuwa ni wakati wa usiku, alitokea mwalimu Shilangale. Kwanza nilishituka na kujiuliza amefikaje Nyambiti kutoka Kinango? Aliniita kwa kina na kuniuliza kwa nini sionekani shuleni. Nilimjibu kuwa niliisha hamia Tallo. 

Mwalimu Shilangale aliniambia kuwa yeye kwa sasa yupo Tallo na hajaniona. Nilimweleza matatizo yangu naye aliahidi kunisaidia kwa namna nyingine.

Siku iliyofuata nilikwenda kuonana na mwalimu Shilangale. Kwa ufupi tu aliniambia kwamba, anwani ya jina langu bado linasomeka halijaondolewa shuleni Tallo. Hivyo basi itabidi nihudhurie masomo ya jioni hapo Community Centre. Yeye atakuwa ananiletea masomo ya kiwango changu. Jambo jingine, nisionekane kule shuleni ili isilete kumbukumbu kwamba bado nipo wakati natakiwa nirudi Kinango.

Nilifanya kama alivyo nishauri, tulikuwa wengi kwa viwango mbalimbali huku nikiendelea kupambana na maisha kama vile sina wazazi. Hata hivyo Mungu ni mwema, nawashukuru wote waliompa hifadhi majumbani mwao kwa namna moja au nyingine, sina cha kuwalipa ila Mungu pekee ni muweza.

Muda wa kumaliza masomo ulikuwa umekaribia. Mwalimu Shilangale alinipa muongozo mzima ni jinsi gani nitaufanya mtihani wangu wa kumaliza masomo. Siku ilipofika sikuwa peke yangu tulikuwa wengi. Tulifanya mitihani yetu yote bila hili wala lile.

Wakati wote wa kusubiri matokeo. Sikuacha kuhangaika, mara kwa mara nilikuwa narudia kukumbuka wosia wa shangazi yangu Gwalihwa kwamba tabu na shida zitanivaa lakini uvumilivu wangu utanifikisha pazuri.

Shule za enzi hizo Alihamdulillah ilikuwa ni ujanja na utundu wako mwenyewe. Nilianza kujiendeleza kwa wasamaria wema waliokuwa na fani tofauti tofauti. Kama vile ufundi cherehani ingawa nilikuwa na uelewa kidogo wa fani hiyo, ambao nilikuwa naibiaibia kutoka kwa baba yangu kabla hajabadilika. Msamaria mwema Bw. Abdallah Rashidi Shunulla, alikuwa ni fundi mahususi, alinichukua na kujiendeleza. Namshukuru sana kwani katika safari yangu ya maisha ufundi huo ulisaidia sana. 

Ufumaji wa vitambaa huu nao kwa kiasi kidogo niliupata kutoka shuleni Kinango, halikadhalika uandishi wa herufi sign writers. Fani hizo mbili nilipata bahati ya ya kuchunukiwa na bwana mmoja ambaye alikuwa ni mwajiriwa, namkumbuka kwa jina moja tu la Feruz, kazi yake ilikuwa ni kufungulia na kufunga maji. Pia alikuwa ni fundi bomba. Mbali na hayo alikuwa na ujuzi wa ufumaji wa aina mbalimbali. Hivyo basi huyo alinifundisha ujuzi huo kwa moyo mmoja.

Ujenzi na useremala, vyote nilitoka navyo shuleni Kinango. Huo nao nilijiendeleza mikononi mwa fundi Said mzaramo. Wote hao nawashukuru sana.








****Shinyanga.

Muda wa likizo ulitimu, nilifunga safari hadi Mgodini Mwadui, ambako nilifunga ndoa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. Gharama zote kuhusu ndoa hiyo nilidhaminiwa na rafiki yangu, anbaye alikuwa ni Meneja wa Super Market.

Baada ys siku mbili tatu, niliondoka na mke wangu hadi nyumbani Nyambiti. Nilionekana mimi ni muasi wa dini eti kwa sababu, ndoa ni ya kiserikali na pia utofauti wa imani. Pia mke wangu aliitwankafiri. Yote haya yalishikiliwa bango na shemeji yangu wa kiume.

Nilirudi Mwadui kujiandaa zaidi kwa safari ya kurudi Dar es Salaam. Pamoja na hayo palikuwa na maelewano ya kwamba, nitarudi kumchukua mzazi mwenzangu. Nikiwa katika mazungumzo hayo, walitokea watoto wetu  wa kike na kiume ambao walilia niondoke nao. Sikuwa na jinsi, Niliondoka nao chini ya ulezi wa huyu alipachikwa jina la ukafri. Mtoto mkubwa wa kiume alibaki na bibi yake ambaye ni mama yangu mimi. Ndiye aliye mlea tangu huko nyuma.

Maandalizi yalipotimia, nilirudi Nyambiti kumchukua mke wangu wa kwanza. Lakini hakuwa tayari kuondoka. Alidai kuwa anahitajika aende Nassa kwa mama yake mkubwa kwani anamuhitaji. Nilihisi kuwa lazima kuna namna, kuna jambo. Niliamua kuondoka, watoto niliwaacha  Mwadui kwa huyo aliyeitwa kafiri.

Mke wangu wa pili, kabla sijamchukua kumleta Dar es Salaam. Nilipewa taarifa kuwa Mtalaka wangu alikwenda Mwadui kadi nyumbani kwao. Wakati huo tayari alikuwa na uja uzito wa kwanza. Lakini, ugeni huo ulizua kutofahamu kwamba Mtalaka wangu ameenda kumloga huyu mke wa pili. Hii yote ilitokana na baba Mkwe, kwani alikuwa ni mpenzi sana wa mambo ya wataalamu wa kienyeji.

Hata alipozaliwa mtoto kulikuwa na mabezo kutoka kwa wifi yake kwamba amezaa katoto gani keusi hivyo. Haya yalijenga kinyongo kwa mke wangu wa pili Mkafiri. Lakini yote niliyachukulia ni ya kawaida tu. Kwani ndiyo tuliyiumbiwa, kumsifia kwa ubaya au kwa uzuri, iwe ni kwa matani ama kwa dhati.


****Dar es salaam.

Baada ya siku kadhaa nilipata taarifa kuwa mdogo wangu pamoja na kafiri wangu wamepatikana na upotevu wa fedha za kampuni kwenye vitengo walivyokuwa wanaviendesha. Rafiki yangu aliye nidhamini kwenye ndoa alinishauri. Mdogo wangu aondoke ionekane ametoroka. Kampuni haitahangaika kumtafuta, bali upotvu huo itachukulia ni upotevu wa kawaida. Huyu Kafiri wangu kiwango ni kidogo sana watamkata kwenye malipo yake ya mshahara. Hata hivyo niliamua aache kazi na anifute Dar es Salaam.

Wakati huo yeye Kafiri na watoto wangu niliwaacha kwa afande rafiki yangu. Ulianza kutokea mfarakano kati yake na mke wa afande huyo. Yote yalitokana na urafiki uliokuwepo kati ya mke wangu wankwanza na huyo mke wa afande rafiki yangu. Hivyo lilijengwa jungu la mateso ya watoto.

Pamoja sikuwa na makazi ya uhakika, ilinilazimu kuwachukua na kukaa nao kwa kaka yangu  kambini Jeshini. Ilibidi niwe mvumilivu kwa kila hali. Nilikuwa na kazi kubwa ya kila kambi kuulizia nyumba zilizo wazi.

Kwa bahati kulikuwa na afande aliyekuwa anakaa kwenye nyumba za kawaida, alipewa uhamisho. Nilimwendea kiongozi wangu wa juu aliyenipa msaada wa kuipata nyumba hiyo. Hivyo ilitolewa amri kuwa, nyumba hiyo nitainhia mimi.

Nilimshukuru sana kiongozi huyo pamoja na kaka yangu, aliniwezesha usafiri wa Jeshi kunihamishia mahali pangu.  Kuhusu makazi nikawa sina wasiwasi tena. Bali sasa ikawa kazi ni kazi tu. Wakati huo kiongozi wangu mkuu alikuwa ameniagiza kuandaa mchoro wa jengo kwa ajili ya ofisi za Mkurugenzi. Nilifanikiwa kuuandaa na kisha nilimkabidhi.

Baadae nilitakiwa kwenda kutoa mafunzo chuoni Moshi mkoani Kilimanjaro. Kabla sijaondoka, niliomba siku saba nipitie Nyambiti. Nilimkuta mke wangu wa kwanza ameajiriwa kwenye kiwanda cha Pamba (Nyambiti Ginnery). Nilipata jibu kuwa ndiyo maana alihitajika aende kwa mama yake mkubwa Nassa.

Meneja alikuwa ni mtoto wa rafiki yake na baba yangu. Alikuwa ni mnyenyekevu kwangu baada ya kumwambia mimi ni mtoto wa nani. Nilimuonesha vielelezi vya ndoa yetu ambavyo alikubaliana navyo. Alimwachisha kazi mara moja, kwani alithubutu kudanganya kuwa hajaoolewa.

Baada ya kufika chuoni Moshi. Nilitafakari sana kuwa mwisho wetu ni nini? Niliamua bora tuachane kwa wema. Niliandika taraka nikazituma hadi ofisi ya BAKWATA Nyambiti mahali alipo kabidhiwa. Baada ya siku chache nilipata hali halisi jinsi ilivyo mfikia talake yake. Wazazi wa pande zote waliitwa kushuhudia tukio hilo lililo fanywa na Katibu na kamati yake.

Mtalaka wangu alilia sana na  alimuomba mama msamaha, kwani alikuwa kaponzwa na mama yake. Lakini ilikuwa ni kazi bure, kwani hakuweza kunifuata tena. Lakini baada ya muda fulani kupita, mtalaka wangu alifika Dar es Salaam, lakini alifikia nyumba ya wageni. Madhumuni ya safari yake  ilikuwa ni kuwachukua wanae kwa madai kuwa watoto walikuwa wnateseka kwa kazi za ndani. Mtoto wangu kiume alikataa kuodoka na mama yake. Huyu mwingine wa kike aliondoka na mama yake akiwa darasa la kwanza.

Mtalaka wangu alizidi kuyabeza maisha yangu kuwa ni duni. Hayalingani na wengine tulio kuwa nao mgodini Mwadui. Kwamba wana maendeleo makubwa, wana majumba nakadhalika. Haoni sababu ya mimi kuwepo mahali pasipokuwa na pesa. 

Aliye wapa wao ndiye aliyeninyima mimi. Kama nimeandikiwa hapana, haiwezi kubdilika ikawa hapana. Yaliyo ya Mungu lpe Mungu na shetani, mwachie shetani bana. Hayo yalikuwa majibu yangu kwa mtalaka wangu.

Lakini baadae niligundua kuwa, ubezaji huo ulitokana na mafunzo ya huduma ya wagonjwa (Nurse) aliyapata baada ya kumtalaki, alikuwa pamoja na dada yangu mtoto wa mama mdogo; basi yeye alijichukulia yeye zaidi, mimi si kitu kwake.

Hata hivyo baada ya mafunzo hayo, hakuwa mtulivu, alikuwa mara hapa, pale hatimaye alishika uja uzito aliopewa na kiongozi mmoja wa dini, alimzalia mtoto wa kike. Kiongozi huyo hakudumu alifariki. Mwisho labisa aliolewa na bwana mmoja ambaye tulikuwa wote utotoni. Wazazi wake walikuwa wamepanga nyumbani kwa mama yangu mdongo. Naye pia alimzalia mtoto wa kike, halikadhalika bwana huyo nae hakudumu alifariki.

Mkafiri wangu alishika uja uzito tena kwa mara ya pili. Lakini hakuta tena kuwa mtoto mwingine. Alijitahidi sana kuitoa hiyo mimba lakini ilishindikana. Hapakuwa na sababu tena bali alisubiri alicho kitaka Mwenyezi Mungu, hadi alipo jifungua mtoto wa kike kwa mara nyingine. Hawakukosea walio sema kuwa, 'malipo ni hapa hapa Duniani'.

Alijifungua salama salimini, lakini ghafla alishikwa na maumivu ya miguu. Tatizo lilikuwa linampata mara jua linapo zama yaani jioni. Panapo pambazuka maumivu nayo yanapotea. Katika kuhangaika stafu wangu alinipeleka hosiptali ya JUWATA Shauri Moyo Ilala. Alipata matibabu ya kina yaliyo tuliza maumivu aliyokuwa nayo.

Wakati huo nilikuwa na wapwa zangu watatu walio telekezwa na baba yao mdogo. Niliamua kuchukua likizo. Nilipo fika Shinyanga kafiri wangu alibaki na wanae hao wawili. Mimi niliendelea na safari hadi Nyambiti kuwapeleka hao wapwa zangu. Baadae nilirudi Shinyanga, nilimkuta anaendelea vizuri kwa madai kuwa ni msaada wa baba mkwe kwa njia za kienyeji.

***Shirika la Umeme:

Mkafiri wangu alipotoka Mwadui, hakuwa na kazi takribani miaka miwili. Katika kupitia magazeti, kulikuwa na tangazo la nafasi ya kazi katika shirika la umeme, nafasi ya uhudumu wa ofisi na mapokezi. Niliandika maombi mimi mwenyewe na kisha nikapeleka panapo husika.

Baada ya siku kdhaa kupita, nikuta tangazo linawahitaji  kwenye usaili waliomba nafasi hizo kwa tarehe ya siku hiyo. Nilishituka kuliona tangazo hilo, kwani barua ya  wito sikuletewa.

Nilipo fika kwenye ofiisi zao, nilitakiwa kutoa barua ya wito. Niliwajibu kuwa hakunitumia bali nimeona kwenye gazeti. Alitokea afisa mmoja, alinipa karatasi ambazo zilikuwa ni kwa ahili ya vipimo vya afya. Alinipa kipa umbele wa masaa. Yaani itakapofikia saa nane mchana, niwe nimekamilisha kila kitu. Wakati huo ilikuwa saa nne asubuhi.

Nilimchukua mke Kafiri wangu hadi Mnazi mmoja. Kama umeandikiwa ndiyo haiwezi kuwa hapana. Nilikamilisha kila vipimo ndani ya saa moja tu. Nikarudi hadi kwenye shirika hilo, bahati nzuri nilimkta afisa aliyenikabidhi nyaraka  za vipimo. Alishangaa sana hakutegemeakama ningefanikiwa.. Kisha aliniambia mimi niondoke, Kafiri wangu abaki pale kwani tayari ajira ameisha ipata.

Jioni tulipo kutana nyumbani, akinifahamisha kuwa amepangiwa sehemu ya mapokezi. Kwake haikuwa shida kwani tayari aliisha chukua mafunzo ya Uhazili Secretarial Duties hapo Mwadui. Aliendelea na kazikazi hadi kipindi cha majaribio kilipita na akathibitishwa ajira.

Zilitokea nafasi za kwenda chuo kwa masomo ya Labour Duties ngazi ya cheti ambayo yalikuwa ni mwaka mmoja. Nilikubaliana naye, nilibaki na watoto ili akaongeze ugali. Nilikuwa najali sana maendeleo ya kielimu.

Haikuchukua muda baada ya kumaliza mafunzo. Zilitoka nafasi tena kwa ajili ya mafunzo hayo hayo kwa ngazi ya Diploma ya juu. Kafiri wangu alikubaliwa kuhudhulia mafunzo hayo. Lakini kwa bahati mbaya sana, hakuweza kwenda kutokana na maradhi yaliyo msibu. Hata hivyo nafasi yake ilihifadhiwa mpaka muhula uliofuata. Nilibaki tena na watoto, kipindi chote cha miaka mitatu.

Nilikuwa msaada mkubwa kwake, nilimsaidia sana katika kipindi cha field. Kumpatia data, kumchapia na kumtengenezea kitabu kuhusu tafiti alizopitia na kadhalika. Kablabya mwaka mmoja wa kumaliza mafunzo yake. Nolichaguliwa kuhudhuliwa mafunzo ya kupandishwa cheo ngazi ya nyota tatu, Mrakibu Msaidizi 'Assistant Superintendent'. Haikuwa shida kwangu kwa kuwa Chuo kilikuwa mkabara na kambi, kila jioni niweza kuwajalia hali na hata siku mwisho wa wiki niliweza kulala nyumbani.

Mke wangu alipo maliza mafunzo, alipandishwa cheo, akapewa gari na dereva na mshahara ukaoanda mara dufu. Hapo ndipo mabadiliko yalianza kuonekana. Safari za kwenda semina huku na kule zikashamili. Alikuwa hajui kujipodoa, sasa ikawa ni balaa. Mikanda ya ngono ikaletwa chumbani, eti ilikuwa ni moja ya semina na baadhi aliyafanyia  uhakiki kwangu. Nilitafakari sana, tumetoka wapi, sasa tulipo ni wapi na tunakoelekea ni wapi?

***Ushirikina***

Kuna siku sikujisikia kwenda kazini. Wakati huo niliisha maliza mafunzo na tayari cheo niliisha pata. Hapo tupo kambini Mtoji Kijiji kwenye nyumba ya hadhi yangu. Nilipata hisia ya kutokuwa na imani na chumba chetu. Niliamua kufungua kabati la nguo, upande wa mke wangu. Nilichokikuta sikuamini macho yangu.

Nilikutana na kitambaa chekundu kimekunjwa vizuri kabisa. Nilishituka, nilitulia kama sekunde kadhaa. Nilikifungua, kwa ndani nilikuta hirizi ya kitambaa cheusi, imefunikwa kwa kitambaa cheusi na karatasi yenye maandishi ya Kiarabu yaliyoandikwa kwa kalamu ya kawaida ya wino mwekundu.

Karatasi hiyo ilikuwa ni Talasim ambayo ilikusudiwa kuniharibu akili. Nisiwe kakli yoyote kwa mke wangu. Yeye awe ni mtawala wa nyumba. Niwe mtu wa kukaa ndani mara ninapo toka kazini. 

Niliichunguza kwa makini talasimu ile. Niligundua kuwa apigwa yaani kaingizwa mjini au kadanganywa. Talasimu kwa ufahamu wangu, huandikwa kwa kutumia onyoya wa ndege, pia wino utmiakao ni zafarani nyekundu. Vilevile jina langu alilikosea badala ya Ahmad liliandikwa Mohamed na ubini wa mama mzazi uliandikwa  Hawa.

Sikuona sababu ya kukaa kimya, jioni alipo rudi nilimuuliza kulikoni. Majibu yake yalikuwa eti ni kwa ajili yake yeye mwenyewe huko kazini kwake. Nilimpa onyo iwapo ataendelea na tabia hiyo basi mimi ipo siku nitamkimbia.

Halikuwa tukio hilo tu, hata huko nyuma kabisa mambo mengi alikuwa anakimbilia kwa wataalamu mbadala. Niliwahi hata kukataa kutoa malipo kwa ajili mtaalamu alieye dai katokea Songea na alijiita jina la Songea. Mbali na hayo, alidiliki hata kuniandalia maji ya kuoga yasiyo ya kawaida.



***Niliisha kufa vitani***

Ulipita muda wa miaka takribani mitano sita, sikuwa nimefika Nyambiti wala kuona na binti yangu huyo aliyeondoka na mtalaka wangu, hata yule wa kiume pamoja na wengine wote.

Nilijiandaa kwenda  nyumbani Nyambiti, nilituma taarifa ya ujio huo. Siku nafika Nyambiti, nilikuta baadhi ya familia yangu inanisubiri, mmoja wao alikuwa ni huyo mtot wangu wa kike akiwa ni binti mkubwa tu. Nilipo telemka kutoka ndani ya gari, mara binti huyo alinivamia na kunikumbatia. Lakini alikuwa analalamika kwamba, aliniita na kusema "baba, baba, baba, niliambiwa kuwa uliisha kufa baba huko vitani Kagera."

Kilio chake kilinikumbusha wakati wa vita hivyo. Yalifanyika makosa. Askari aliyekufa majina yetu yalifanana hata ubini, hali kadhalika namba za Jeshi zilifanana. Zilianzia na tarakimu ya nane na zilizofuata pia isipokuwa tarakimu ya mwisho ndizo zilitofautiana. Hivyo nguo zake zililetwa kimakosa nyumbani. Hata hivyo haukuwa utaratibu sahihi, sijui kwa nini ilifanyika hivyo. Nilizichukua nguo hizo nikazipeleka mahali husika kwa hatua zaidi.

***Ramani ya jengo***

Nilipo kuwa bado nipo chuoni, nilipata fununu kuwa, mchoro au ramani ya jeongo la ofisi za Mkurugenzi umekubalika na jengo liko mbioni kumalizika, nilifarajika sana.

Siku kadhaa zilipita, kulikuwa na tukio la uhaini ambao walitoroka gerezani. Wakuu wa vituo na maafisa walifika katika tukio. Nikiwa askari wa cheo cha chini koplo, ambaye sikustahili kujumuika na maofisa; lakini niliamriwa kuambatana nao.

Maafisa walikuwa wananishangaa, kwani kwenye tukio sikuonekana najihusisha na lolote, bali yangu yalikuwa ni macho na kushika maelezo ya mwelekezi. Kiongozi mkuu alidiriki kunihoji kwa nini sijishughulishi. Nilimjibu kuwa kila kitu kipo kichwani mwangu.

Usiku mzima wa siku hiyo, ilikuwa ni kazi moja tu ya kuukanilisha mchoro mzima wa tukiopoja na vielelezi vyake.  Asubuhi yake nilitakiwa kuukabidhi kwa Mkurugenzi. Niliwakuta maafisa niliowaona jana yake. Nilimkabidhi, nilibaki nimesimama nasubiri amri ya mwisho. Mmoja wa maafisa aliniamru niondoke, lakini kauli yake ilivunjwa na amri ya Mkurugenzi. Niliamriwa niketi. Niliamua kukaa  nyuma yao.

Mkurugenzi aliagiza mchoro wabgu kila mmoja aupitie kulinganisha na michoro zaidi ya miwili iliyo wasilishwa. Baada ya hapo kila mmoja alikubaliana na mchoro wangu. Wote walistaajabu, nimekumbukaje mazingira yote yale, wakati nilikuwa sijishughulishi na chochote. Walikuwepo walionung'unika kwa nini sipewi cheo, wanazidi kunitumia tu. Basi mchoro wangu ulipitishwa kwa asilimia zote, ulichukuliwa na ulitumika mahakamani.

Mungu sio Makaranga, siku chache baadae zilitoka nafasi za kusomea vyeo, lakini jina langu halikuwemo. Sikufa moyo, nilimtanguliza Mungu kwamba ipo siku itakuwa ndiyo. Maajabu ni kwamba, ndani ya kipindi cha mafunzo hayo, nilitunukiwa cheo cha Sajenti bila kuyasomea.

***Mafunzo***

Binadamu hawana dogo, hilo likawa ni nongwa. Wengine walinisema mimi msomi, mara mtoto wa afande nakadhalika. Sikuyajali bali niliendelea na kazi zangu za kila leo bila ya kumdharau mwingine bali ilikuwa ni kwa heshima na kumjali kila mmoja.

Ilifika awamu nyingine tena kama hiyo. Safari hii jina langu lilikuwemo. Nilipofika chuoni niliteuliwa kuwa kiongozi msaidizi wa kombania ya mafunzo.  Kwa wakati tuliokuwa hapo, mara tulihitajika mjini Arusha kwa kazi maalumu. Mimi nilikuwa ni mmoja wa miongoni mwetu. Tulipiga kambi nje ya jiji maeneo ya Olujolo. Huko nako nilipewa madaraka ya uongozi, kazi yangu ilikuwa ni kupanga ratiba za utendaji na kufanya mamaresho ya hali nzima ya maisha ya kikosi chetu. Kazi ya operesheni ilifanyika vizuri na kuleta sifa kwenye chuo.

Chuo kilinifahamu tangu wakati wa mafunzo ya awali kutokana na halakati nilizo kuwa nazo. Hivyo hata kipindi hiki sikuacha maono yangu yapotee. Kwa kuwa nilikuwa ni kiongozi msaidizi, niliamuru eneo la mabweni tuliyoyatumia wana mafunzo ya S/Sajenti, kuyang'oa maua yote. Kisha tulitafuta miche ya minyanya tukapandikiza.

Lilikuwa ni gumzo sisi kwa kwani tumekwenda kinyume na utaratibu wa chuo, hasa pale mkuu wa chuo atakapo fanya ukaguzi wake wa mwezi. Hata hivyo niliwatoa hofu. Niliwaambia wenangu kuwa hilo waniachie mimi, nitabeba misalaba yao.

Lisemwalo lipo, au lipo njiani. Kweli ilifika kipindi cha ukaguzi wa mkuu wanchuo. Kilicho nitoa shaka, kipindi hicho nyanya zilikuwa zimesitawi vizuri sana, zumeweka matunda yake makubwa na zilikuwa zinaelekea kuiva.

Mkuu wa chuo alipofika eneo letu, na mimi nikiwa ni miongoni niliyeongozana naye. Ghafla alisimama. Wakati huo nilijaribu kumuiba iwapo amekasilishwa na hali hiyo, lakini nilikuta anatabasamu. Alilizunguka eneo zima alicho kikuta ni nyanya.

Katika kikao chake na wanafunzi, aliagiza wengine waige kwetu. Tulisimamishwa viongozi na alitupa sifa iliyo sitahili.

Kingine kilicho waacha midomo wazi, zilipatikana taarifa kuwa, tepe za vyeo ni chache hazitolezi kwa wanafunzi wote. Hivyo basi watavalishwa wachache kwa niaba ya wengine. Niliamua kutengeneza tepe za nyuzi na vitambaa na rangi kwa vyeo vyote.

Siku ya mwisho baada ya kutolewa tamko la kupanishwa vyeo, ilikuwa ni kazi ya haraka ya kuvishana tepe za vyeo vyetu. Kwa muda mchache tulionekana wote sawa. Kilimshangaza Mkuu wa chuo. Aliniamutu kabla sijaondoka  nimtengenezee tepe kwa ajili ya maafisa wake na yeye pia. Mwisho aliniambia, kweli mimi ni Fujo. 

Wakati nilipo kuwa nimefikia cheo cha Mkaguzi Mdogo 'Assitant/Inspector, nilikuwa miongoni tulio teuliwa kuchukua masomo ya lugha ya Kijerumani mbali na wale wengine walichaguliwa katika masomi ya ya lugha ya Kifaransa. Masomo yetu yalifanyika katika kituo cha Goithe Institute Dar es Salaam, katika ngazi ya awali ya miezi mitatu. Baadae tuliendelea na ngazi ya cheti kwaya yalikuwa ni maandalizi kwamba, wale watakao faulu watapata nafasi ya kupelekea Ujerumani. Darasa langu tulikuwa arobaini na tano. Nilibahatika kuwa wa kwanza kufaulu, nilifuatiwa na Sister Monica kutoka Peramiho. Darasa lililofuata walifaulu wawili pia, Andreas Mfilipino na Luteni Kapongo. Hao ndio tulio bahatika kwenda Ujerumani.


*Kitengo cha takwimu.

Nilikuwa kuwa kitengo cha Takwimu cha Makao Makuu. Tangu huko Shinyanga kazi za kiofisi zilikuwa hazinipigi chenga, mbali na maeneo maalumu ya kazi zangu zingine. Katika kitengo hicho kulikuwa na kiongozi Mkaguzi na msaidi wake Sajini Meja. 

Kazi zote za kiofisi zilikuwa mimi ndio mtendaji. Kuandaa taarifa yaya mwezi, robo mwaka, nusu na robo tatu ya mwaka na hata mwaka mzima. Michoro mbalimbali kama vile Graphs nakadhalika.

Ilifika wakati viongozi hao waliondoka kwenda masomoni. Swali lilikuwa, nani ashike nafasi zao. Maafisa wa vitengo vingine walitegemea kwamba watateuliwa. Lakini ilikuwa ni kinyume. Mkurugenzi aliamuru pamoja na usajenti wangu nitabaki na kushika nafasi hiyo. Kinachotakiwa ni taaluma na busara tu.

Kulikuwa na mambo kadhaa ambayo kutokana na cheo cha Sajenti ilikuwa ni kikwazo kwangu kuyafanya, ndiyo maana maafisa wengine walitamani sana nafasi hiyo. Lakini Mkurugenzi aliagiza nifanye kila kitu, yale ambayo yatahitaji kupitishwa na afisa, basi nimpelekee yeye mwenyewe atayasaini hadi viongozi wangu watakapo rudi.

Viongozi wangu walipo rudi, aliye kuwa msaidizi alihamishiwa Benk Kuu. Aliyebaki alifanya mikakati ya kuhama, kwa vigezo kuwa hana taaluma hiyo ya takwimu kwani hakufaulu alipokuwa chuoni. Ila mwenye taaluma hiyo ni mimi. Aliamriwa asubiri hadi nitakapo kuwa mkaguzi (Inspekta).

Ilichukua muda mfupi mara nilichaguliwa kuwa kuhudhuria mafunzo ya ukaguzi. Mafunzo yalifanyika Dar es salaam. Nilichaguliwa tena kuwa kiongozi wa darasa na mrakibu wa mafunzo. Tulikutana wengi ambao tulikuwa wote huko nyuma. 

Kulikuwa na kejeri ya waliotoka Chuo Kikuu kitengo cha sheria, walijiona wao ndio wao kwani walisamehewa wasifanye mitihani ya sheria. Waliagizwa waunde makundi ya kujisomea (group discussion). 

Sikutaka kuwa kwenye makundi hayo kutokana na kejeri zao. Niliamua kujenga kundi langu ambalo lilijumuisha waliotoka Zanzbar na wengine wachache. Nilijiwekea muda tofauti na wao. Badala ya saa mbili usiku hadi.saa nne kasorobo usiku. Kwangu ilikuwa ni saa kumi na moja jioni, hadi saa kumi na mbili jioni. 

Nilichukua jukumu la kutafasiri masomo kutoka kiingerza hadi kiswahili kwa wale walikuwa na uwezo mdogo wa lugha. Uzuri wote tulifanya vizuri.

Mkufunzi wa somo la Sheria ya Ushahidi alitupa angalizo kuwa. Mitihani yake siyo ubuyu. Hakuna atakae vuka nusu ya ufaulu. Lakini alipatwa na kigugumizi, katika mtihani wake wa kwanza, mimi nilipata alama tisa ya kumi, mwenzangu alipata asilimia nane ya kumi.

Mkufunzi huyo alitaka kutufahamu tunafananaje, kwani mtihani tuliutunga tukiwa pamoja yeye? Kuania hapo mkufunzi huyo alikuwa akifika darasa letu na alitoa muhitasari tu kisha kazi iliyobaki aliniachia, niliifanya bila kasoro. Hata hivyo hakuridhika alijaribu kunidadisi  elimu yangu. Alikuta nimepitia mambo mengi, ufundi magari daraja la pili, ufundi cherehani, uchoraji wa ramani ngazi ya cheti, ukatibu muhitasi ngazi ya cheti, sheria cheti, lugha ya kijerumani Diploma, takwimu Diploma. Alitoa ushauri kwa nini nisihamie chuoni.

Baada ya kufuzu mafunzo yangu hayo, nilirudi katika kitengo changu, nikiwa na mikakati ya kuhamia vituoni ama mikoani kabisa. Lakini jitihada zangu ziligonga mwamba. Matokeo yake nilikabidhiwa ofisi rasmi. Kiongozi wangu ndiye aliyehamishwa, alipelekwa kituo cha Masasi.

***Likizo.

Muda wangu wa likizo ulifika. Nilikwenda nyumbani Nyambiti. Baada ya siku kadhaa nilizopumzika, nilipewa kazi ya kufuatilia vitu vya mdogo wangu aliyekuwa ameajiliwa mgodini Mwadui. Maagizo hayo niliyapokea kutoka kwa mzazi wake ambaye alikuwa ni mume wa mdogo wake na mama yangu.

Ilikuwa ni jioni ya saa kumi hivi, nilikuwa nimekaa nje ya mgahawa uliokuwa jirani na mzazi huyo. Kikubwa, nilikuwa nafikiria juu ya safari ya kwenda Mwadui, niende ama nisiende? Mara gari lilifika ambalo ni la abiria, dereva wa gari hilo alikuwa ni huyo mdogo wangu, pia gari lilikuwa ni mali ya mzee wake.

Wakati huo  wimbo wa Matimila wa kifo hakina huruma, ulikuwa ukichezwa kwenye radio. Mdogo wangu alinifuata nilipo kuwa nimekaa, aliniambia tuondoke. Aliniomba niendeshe gari lakini mimi nilimkatalia.

Tulipofika sehemu inaitwa Jojilo, tulipata ajali wakati anaendesha yeye mwenyewe. Gari liliangukia upande niliokuwa nimekaa kwenye siti ya kondakta. Ajali ilisababisha kifo cha mtoto mchanga wa miezi mitatu. Kulikuwa na mdogo wetu mwingine, yeye alipata majeraha sehemu za ubavuni. Mimi pia niliathirika ubavu wa mwisho kushoto.

Taarifa iliwafikia nyumbani katika sura tofauti. Kwani walipewa habari kuwa mimi nimeisha kufa. Ilibidi mdogo wa mwenye gari afuatilie. Alitukuta zahanati ya Ngudu, tayari tulikuwa tumeisha hudumiwa. Na wakati huo nilikuwa najaribu kuzungumza na askari wa usalama barabarani kuweka mambo sawa. Hivyo safari ya kwenda Mwadui ikaishia hapo. Muda wa likizo ulipo kwisha nikarudi zangu Dar es Salaam.

Baada ya siku kadhaa, nililetewa habari kuwa baba yangu mzazi ni mgonjwa. Ilibidi niombe likizo fupi. Nilifika Nyambiti, nilimuomba mdogo wangu huyo niliyepata nae ajali, anisaidie kiasi cha pesa. Lakini nikawa nimejipalia mkaa wa moto. Nilipokea matusi, kauli ya kubeza uaskari wangu, kama uwezo ninao basi niyasimamishe magari yao yasitembee nakadhalika.

Nilikereka sana, niliamua kutokanyaga kwenye mji wao, na kweli nilifanya hivyo. Mdogo wake mama, ambaye ni mama yake yeye, alishituka sana alipooa siku zinazidi kupita sujaonekana nyumbani kwake. Kwani nilikuwa ni kipenzi kwake, wasiojua walikuwa wakichulia mimi ni mwanae mkubwa.

Alinifuata na kutaka kujua kulikoni. Sikumficha kitu, nimweleza kwa uwazi tupu. Alinisihi nitulize hasila zangu, jambo hili atalifikisha kwa bibi yetu na atatuweka sawa.

Zilipita siku kadhaa bila ya mwenzangu kufika kwa bibi yetu kwa kisingizio kuwa kazi zimemtinga. Matokeo yake nilitakiwa niende kwao nikaonane na baba yake mzazi. Nilipofika huko nilimkuta mama yetu mwingine mdogo. Alituongoza hadi ndani ya ghala, alimuonesha mwanae mahali alipokuwa ameficha kitu. Alimwambie achimbe kwa sululu. Alitoa kopo tukaenda nalo hadi ndani.

Alilifungua kopo hilo na  kutoa vipande vya alivyo dai kuwa ndivyo nilivyokuwa nampelekea. Alinikabidhi na kudai kuwa, hawezi kunidhurumu, ila eti mimi nilifanya vibaya kumpelekea machupa. Mama mdogo aliniuliza iwapo ni sahihi.

Ukweli nilijizuia sana, lakini niliumia sana. Nilimwambia mama mdogo achukue na tuondoke. Nilipofika nyumbani kwa bibi, nilimuuliza mama mdogo. Inawezekanje kukaa na madini ya thamani kwa miaka yote takribani kumi na ushehe?

Mbali na hilo, nilikuwa nakutana na mtaalamu wake wa kienyeji, alikuwa ananiambia kuwa walikuwa Arusha na wamefanikiwa kuuza mali, siyo chuni ya mara nne. Hapo hapo alikuwa akiniambia kuwa kuna trekta kaninunulia na alinionesha kwa macho yangu. Pia gari la abiria tulilopata nalo ajali nishea na mimi nikiwemo. Kulikuwa kuna haja gani kunishahidia hayo?

Nilimwambia mama mama mdogo kuwa, hapa nimeisha dhurumiwa, nilimletea kitu sahihi, leo narudishiwa kitu feki. Baada ya siku mbili kupita nilikwenda mkoani Shinyanga kwa watu nilokuwa nawafahamu kwa shughuli hizo kwa ajili ya kuhakiki. Lakini jibu lilikuwa negativu. Ingawa kulionekana vipande viwili vidogo ndiyo Postivu. Lakini havikuwa nasoko kutokana na udogo wake.

Niliamua kurudi navyo Dar es Salaam, ambako tulionana na mtu mwingine tuliye kuwa nae Mwadui. Alidai kuwa ana watu vitauzika tu. Halikadhalika nae akalala navyo mbele.

Kilitokea kifo cha Robert Elias (Pilimi). Alikuwa ni mtoto wa mke mdogo wa baba yangu. Pia alikuwa mchezaji wa klabu ya Simba kwa wakati huo. Tulijitokeza vijana wa Nyambiti, baada ya kuliona tangazo lake kwenye gazeti la mfanyakazi, kwamba ndugu wanahitajika.

Tulifanya juhudi za kuusafirisha mwili wake, kwa msaada mkubwa wa aliyekuwa Mh. Mbunge wa Sumve Bw. Ndassa. Kura iliniangukia mimi ya kuusafirisha mwili wake hadi Igoma mahali alipozikwa.

Baada ya mazishi, mdogo wangu aliyenikashi alinomba tuambatane naye hadi nyumbani kwake Kisesa, kwamba ana mazungumzo na mimi.  Pamoja nilikuwa bado na duku duku la kukashifiwa na kufanyiwa dhuruma, niliukubali wito wake.

Aliniambia kuwa, kabla baba yake hajafariki, alimwachia maelekezo mojawapo ni kuhusu haki yangu iliyoko kwao inabidi anikabidhi. Hakuniambia ni kiasi gani, na sikuwa na ile hali ya kutaka kujua, kwani niliisha dhurumika.

Tuliahidiana kuwa ajiandae hadi nitakapo rudi kwa ajili hiyo tu. Kwani kwa wakati huo muda wangu ni mdogo sana. Niliporudi Dar es Salaam, niliomba likizo kwa minajili hiyo tu. Ndugu yangu huyo alinipokea vizuri tu. Lakini ndugu yangu huyo alikuwa anajihimu kila leo kwa siku nilizo kuwepo pale, alfajiri na mapema, tuliwahi kuondoka nyumbani. Kwa sababu ya kufanya mahesabu na kuchukua fedha kwenye gari la abiria ambalo tulianguka nalo kipindi cha nyuma. Hapakuwa na kazi nyingine, bali tulibaki kijiweni tupiga soga. Jioni tunajirudisha nyumbani.

Siku ziliyoyoma bila lolote kufanyika kuhusu kilicho nipeleka. Ilibaki wiki moja tu niwe kazini. Nilimkumbusha ujio wangu,lakini jibu lake lilikuwa kwamba naweza nikaondoka tu.

Nilishikwa na kichomi. Nilijiuliza, kwa nini kabadilika? Niliwaza mengi, machungu yalijaa moyoni, kwani nilishindwa hata kufika nyumbani Nyambiti kwa ajili ya ahadi yake. Kibaya zaidi, ñilikuwa nimeisha mjulisha baba kuwa nitaenda kulichukua gari alilonipa baba ili tukalikarabati mjini Mwanza. Yote hayo yalikuwa ni pigo kwangu dhidi ya wazazi wangu.

Ilifikia hata salamu ilikuwa ngumu, akawa ananitoroka safari za mjini. Kurudi kwake ilikuwa ni usiku nimeisha lala. Zilibaki siku tatu niwe nimeondoka, siku hiyo alikuwa yupo ndani kajifungia chumbani kwake. Kila aliye muhitaji aliambiwa hayupo yuko mjini. Hata mimi niliamini kuwa hayupo. Kweli kuna usemi usemao 'Mficha maradhi kifo kitamuumbua.'

Baada ya dakika chache, tingo wa gari hilo alifika kumuulizia tajiri yake. Lakini alipewa jibu hilo hilo la hayupo yupo mjini. Mara ghafla aliibuka baada ya kusikia sauti ya tingo wake. Bila ya kucjelewa , alimpa habari kuwa gari limepata ajali, vioo vyote vya upande lilikoangukia na vioo vya mbele vimevunjika.

Basi ikawa sababu kubwa ya kutotimiza ahadi aliyo iweka. Alikataa hata kunipa nauli ya kwenda mjini. Kwa uchungu mkubwa ilinitoka kauli kuwa, iwapo mama yake na mama yangu hawakutoka tumbo la mama  mmoja ambaye ni bibi yetu sote, na mimi kama sikutoka kwenye viuno vya mzee wangu; hilo gari atalifufua vinginevyo asahau.

Mungu si Hamisi, niliamua kuondoka, nilupofika barabara kuu, mara gari LandRover pickup lilisimama na mmoja wa abiria aliamru nipande garini. Sauti iliyo sikika mbele ya gari ilikuwa ni kunisamilia kwa kutaja jina langu. Alikuwa ni kijana tulikuwa nae mgodini Mwadui, pia nilisoma nae. Alinipa ofa ya usafiri hadi mjini Mwanza.

Nilimfuata mjoba wangu, nilimweleza hali halisi. Alinituliza na kuniambia hayo ni mapito tu nisijali. Kesho yake mjomba alisindikiza kituo cha treni, alinipa hela kiasi cha kujikimu na safari njiani.

Kuna lugha isemayo, 'nzela yahobwa ntongi'. Ikiwa na maaa kuwa, Mtanguliaji aliisha ipotosha Dira uelekeo wake. Nasema hivyo kwa sababu, nilipo kutoka Kisesa, nilikitana na askari tuliyekuwa naye pamoja Mgodini Mwadui. Aliniomba nimwachie  vile vipande vya almasi jwamba yeye ana mahali atavipeleka. Nilimwamini nikamuachia. Siku, wiki, miezi bila mrejesho wowote. Kila nilipo muuliza hakuwa na jibu sahihi. Tayari naye aliisha nidhurumu.

***Mabadiriko***

Niliendelea na maisha kama kawaida katika makazi mapya ya Kambi. Ukifika sehemu au maeneo fulani ni wajibu ujenge ukaribu na wenyeji. Jatika sehemu za mapumziko yenye vinywaji ilikuwa ni moja ya makutanio na marejeo ya kufahamina kwa namna moja au nyingine.

Kulikuwa na baa moja ilikuwa ni mkabala na njia ikatishayo kueleke kambini kwetu. Mara nyingi ilikuwa ni kawaida mnapokutana hapo, yeyote atakayepita kuelekea kambini ni lazima atawaona, ndivyo alivyokuwa ananishuhudia mke wangu. 

Hali hiyo ilimfanya mke wangu abadirike tibia, akawa ni mtu wa kunisakama kuwa mimi ni malaya, tena ni mlevi. Aliwalisha sumu watoto wetu na hata badhi ya ndugu zangu ikatokea mimi kuwa mbaya kwao.

Ukweli binadamu siyo mkamilifu, mapungufu yapo. Nilijaribu kufanya suluhu ya jambo hilo pamoja na la ushirikina lakini niligonga mwamba. Nilifika mbali sana katika kufakari swala hilo. Nilijiuliza, kama ni kilevi na kujumuika na watu wa jinsia tofauti, mbona alinikuta nalo huko nyuma tuliko anzia, tena tukiwa katika kipato cha chini, wadhifa wa chini kabisa, lakini hakuwahi kulalamika?

Nilikuja nikapata jibu kuwa, lengo lake lilikuwa ni kuniweka katika maisha ya uzezeta. Niliumia sana rohoni. Mimi sikuwa na ujasiri wowote wa kiushirikana wa kupambana na ushirikina na mambo mengine. Bali nimtanguliza Mungu peke yake. Ni yeye mwenyezi Mungu ndiye aliyeniongoza kwa kila jambo, kila wakati nilikuwa namshukuru na kumuomba zaidi aniongoze katika njia iliyo nyooka.

Mabadiliko yalizidi kuonekana. Utaratibu wa matumizi ya mahitaji pale ndani, ikawa siyo tena mimi na yeye mke wangu. Utartibu ulihamia kwa binti yetu mkubwa ambaye alikuwa Chuo Uandishi wa Habari hapa jijini Dar es Salaam. Akawa yeye ndiye mpangaji wa kila kitu katika mahitaji ya jikoni. Hivyo fungu lote la hela alimiliki yeye.

Jambo jingine lililozidi kunivunja moyo ni kule kusilimu kwake; kutoka kwenye Ukristo na kuingia Uislam. Haikutokea hata siku moja kuwa na swaumu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, wala kuingia Msikitini. Nilijitahidi sana kumwandikia mambo ya msingi ya Imanya dini ya Kiislam, nilimnunulia vitabu mbali vinavyo husu dini ya Kiislam, lakini nilikuwa nampia gita Mbuzi. Hata ushauri wa kaka yake aliuweka pembeni.

Bado aliendelea kuniweka katika hali ambayo ilinichanganya. Pale tulipo fanya tafrija ya binti yetu alipo maliza mafunzo yake ya uandishi wa habari. Tangu mwanzo hadi mwisho wa tafruja hiyo ulifanyika katika misingi ya imani ya Kikristo. Nilitumia jekima sikutaka kuharibu sherehe. Nilifunika kombe mwana Haramu apite.


***Mahusiano mbadala***

Katika kuyawaza yote hayo na kwamba alifanya yote hayo alikuwa hajui kuwa ni opotofu, yaliendelea kunifunika blanketi jeusi. Ukweli ni kwamba binadamu tumeumbiwa kupenda na kupendwa. Ilitokea nikajikwaa, nikaangukia mikononi mwa mtu niliye mpenda nae akanipenda, mbali na alikonihisi mke wangu alikonichukulia bango.

Nilikumbuka, watoto wetu wa kiume walipofanyiwa suna ya tohara, kilichokuwa kinafuata ni kufanyiwa kisomo. Ilionekana hatuna ndoa katika misingi ya Kiislamu. Hiyo ndiyo sababu iliyomsababisha aingie Uislamu lakini haikuwa ni matakwa yake.

Ukubali wake wa kusilimu ulipatikana usiku wa manane, usingizi ukiwa umempalama. Miongozo yote ya dini aliipata kutoka kwa ustadha aliyekuwa na madrasa hapo Kurasini. Jirani yangu alikuwa mmshuhuda wa hili.

Mke wangu aliweka wapambe wa kunifuatilia nyendo zangu. Kwa bahati mbaya au nzuri, siku aliyotonywa na mpambe wake aliyekuwa ni mwalimu wa kike wa shule ya msingi kwamba, aje ashuhudie nikiwa na huyo Mbadala wake. Lakini alipofika eneo la tukio alitukuta tunaelekea stendi ya daladala, tukiwa wanaume wawili na mwanamke mmoja. Angewahi kufika angetukuta tupo baa, ambayo ilikuwa mkabala na saluni ya kike ya huyo mwalimu, huyo dume mwingine alikuwa ni kaka yake na huyo Mbadala wake. Walikuwa wote na mabinti zangu katika Chuo cha Uandishi wa Habari, pia alikuwa ni askari Polisi. Basi ilibidi aamini bila uthibitisho.

Kumbuka huyo ni mke wangu wa pili aliyepewa jina la Kafiri, waliompa jina hilo ni wana Nyambiti. Mambo yake yalikuwa kinyongo kitupu. Utafikiri mmeyamalizà kumbe kaweka rohoni.

Nilipata safari ya kikazi katika kanda ya ziwa. Wakati huyu Kafiri wangu alikuwa kaoneshwa huyo Mbadala wake. Aliwatumia  mabinti zangu kwenda kumkera katika eneo la shughuli zake. Nilimuuliza kwa nini mabinti zetu wamefanya hivyo, lakini alikana kuwa hajawatuma.

Nilipata ajali ya kukowa risasi na dhidi yetu na waasi wa nchi jirani. Nilipomjulisha Kafiri wangu tukio hilo, alijibu kuwa na bado utaokota hata makopo.

Majibu hayo yalinipa upeo mkubwa wa kutafakari na kuchambua moja baada ya jingine. Mwenyezi Mungu aliniongoza, alinipa uamuzi badaka ya kuendelea kazi mkoa uliofuata niliamua nilirudi Shinyanga na kisha niende nyumbani kwa wazazi wangunikapate mawiwili matati.

Kuanzia Ushirombo OCD wa hapo alinipokea vizuri tu kwanza tulukuwa nae katika mafunzo ya ofisa. Nilipofika mkoni Suinyanga , Kamanda wa mkoa na Mkuu wa Upelelezi wa mkoa walinikarimu vizuri sana. Baada ya hapo nilielekea wilayani Maswa. OCD wa Maswa alinipeleka hadi nyumbani Nyambiti.

Familia yangu ilisikikitishwa sana na tukio hilo na hasa mwenendo wa Kafiri wangu. Hadi mama aliniambia kuwa yeye aliisha kata mguu kufika kwangu kwa sababu aliisha ambiwa mimi sina kitu, pale kila kitu ni chake mke wangu. Wazazi wangu walinifariji na yote yaliyo tokea. Waliniambia nimefanya vizuri kupitia nyumbani. Mwenyezi Mungu atakuwa na mimi, safari yangu nitaenda salama kabisa na nitarudi salama.

Tuliwahi kununua eneo la ardhi huko Mlamleni mkoa wa Pwani lenye ukubwa wa ekari tatu kasoro robo. Mwaka wa kwanza tulilima mananasi, viazi vitamu na mihogo. Lakini mwaka wa pili Kafiri hakutaka hata kukanyaga kwenye hilo shamba, sababu eti nimegoma kutoa malipo ya mtaalamu aliyekuja kutengeneza mambo hapo nyumbani kama kinga.

Gongo la Mboto tulinunua eneo kama nusu ekari, tuliinua nyumba ikafikia kwenye madirisha. Lakini ilitokea kutoelewana na majirani kuhusu kuachiana mipaka na njia. Niliamua kupauza, fedha tuliitumia katika matumizi ya nyumbani. Ilipokwisha alilalamika hela imeishaje?

Vilevile tulinunua eneo la ekari mbili Kwembe King'azi. Kama mita mia saba hivi kitoka hapo nilimnunulia Mbadala wake nae eneo la ekari mbili vilvile. Lengo langu ni kujenga na kisha nimchukue mama mdogo ambae hakuwahi kupata hata mtoto ili akae na Mbadala wake. Alipogundua hilohivyo alisusia hakutaka kufika tena.

Basi ikawa vituko juu ya vituko. Mara nikute hirizi ndani ya gari. Niliamua kujiepusha na lolote linalo pelekea kutoa matokeo yasiyo mazuri. Nilikuwa na silaha zangu mbili, zote niliziuza kuepuka mateso.

Kuna kipindi baba.yangu alikua kwa dada yangu huko Mikocheni. Nilimuchukua Badala hadi kwa baba nikamtambulisha pamoja na matatizo yote. Baba aliniamuru nifunge nae ndoa haraka kabla hajaondoka.

***Nahama mji***

Uamuzi wa baba alionipa ikawa ni sababu ya kila tunapo kwaruzana Kafiri hukimbilia kusema ni bora nimuoe huyo Mbadala lijulikane moja. Lisemwalo lipo kama halipo basi liko njiani linakuj. Nilitimiza kauli ya baba. Nilifunga ndoa na Mbadala.

Ilikuwa nijioni ya saa mbili wakati wa chakula. Nilikuta chakula kimeandaliwa, ilikuwa ni wali na samaki. Nilishituka baada ya kuona ni kinyume na kawaida yetu kwamba kila moja hujichukulia chakula kichomtosheleleza. Badala yake nilikuta chakula kimeisha wekwa kwenye chombo changu. Wali uliisha changanywa na mchuzi na kipande cha samaki juu ya ubwabwa.

Nilimwachia Mungu. Nilichota kijoko kimoja tu cha ubwabwa na kuuwek kinywani. Nilipo kimeza, nijisikia maumivu makali sana kwenye koo ma vile vitu vyenye ncha kali vinapasua koo. Sikuendelea tena na chakula. Niliinuka nikaenda zangu chumbani kuugulia maumivu yangu. Bint yangu wa tatu alinifuata chumbani kutaka kujua kulikoni. Nilimwambia kilicho nitokea.

Mara lilianza zogo ndani, nilitoka chumbani nia yangu nitoke nje, Mkafiri wangu alianza kunishika na kunisuka suka na kusema eti mimi nimemwambia yeye mchawi. Katika halakati za kujikwamua mikononi mwake alikimbila kunishika kweny korodani zangu, nilishika kichwa chke ambacho alielekea kuzing'ata kodani zangu. Aliishia kunig'ata meno kwenye paja. Nadhani alikuwa na nia ya kuhasi. 

Nilimsukuma akanguka sakafuni na kujifanya amezimia. Watoto walinigeukia na kudainimemuua mama yao. Niliwaambia huyo anafanya maagizo. Kweli mara kialiinuka, nili0ata upenyo nikatoka nje ambako nilikutana na  na dereva wa Bus la Polisi. Nilimweleza yaliyo nisibu na kwamba nitalla ndani ya gari langu. Akinisihi nikalale ndani kuepusha aibu. Nilikubali nilirudi ndani nikala sebuleni. Palipo kucha niliondokea sebule kama nilivokuwa nimevaa nikaenda zangu kazini. Baada ya ya msaa ya kazi kwisha sikurudi tena kwa Mkafiri, nilienda moja kwa moja kwa Mbadala. Nikawa nimehama  bila ya kuchukua chochote.

Kuondoka kwangu mke wangu kulimpa fulsa ya Kufanya mambo ambayo yalikubalika kuwa ni kweli. Alifika hadi kwa afisa mwenzangu kunishitakia kuwa nimemtelekeza watoto na mwingine amefukuzwa shule kwa ajili ya karo. Bahati nzuri afisa huyo alikuwa na yeye ana tatizo kama la kwangu. Alichokifanya, alimwambia anifuate kwa huyo Mbadala kwa kuwa ni mke halali kwa mujibi wa dini ya Kiislamu.

***Uhamisho Dodoma***

Mwishoe alidanganya ofisini kwa mabosi wake kuwa, mimi mumew nimeridhia apewwe uhamisho wa kwenda Dodoma kwa nafasi ya kuonhoza mkoa. Kisha alimwita dada yangu akamkabidhi watoto kwamba mimi sionekani. Yeye amepata safri ya kikazi kwenda Dodoma kwa siku kadhaa.

Nilimfuata kiongozi wake hapo Magomeni. Nilijitambulisha kikamilifu kwa ushahidi usiotia shaka. Kisha nilimdai anirudishie mke wangu la svyo hatua za kisheria itafuata.

Kiongozi huyo alijaribu kunisihi kuniweka sawa  ili tarifa hiyo isiwafikie viongozi wa ngazi ya juu, kwani matokeo yake yatakuwa ni madhara makubwa pande zote mbili. Anweza akarudishwa akiwa ameteremshwa chei kitu ambacho kitamuathiri kiskisaikolojia, au akafukuzwa kazikwa kuudanganya uongozi.

Kiongozi huyo alikili kuwa maelezo yangu na ushahidi wa picha za ndoa, hati ya ndoa ni ushahidi tosha. Kibaya zaidi hati ya makubaliano yenu ya uhamisho hakuna. Nilimpa muda kuwa nitarudi kesho yake kupata muafaka.

Majira ya usiku nilipata simu kutoka kwa kàka yangu, aliniomba niachane na kile nilicho kikusudia kwani kitaleta fedheha katika familia yetu.. Sikuwa mkaidi nilimtii kaka yangu nilifuta alicho nishauri. Nilijitahidi kila baada ya siku kadhaa nilikwenda kuwaona watoto na kuwaachia kile nilicho kuwa nacho. Mara alitokea dada yangu wa kwa mama mdongo. Alishituka kuniona, aliniambia amekuja kuwaona watoto baada ya kujulishwa na Mkafiri kuwa watoto hawana chakula wala pesa.

Nilimwambia  ahakikishe yeye mwenyewe aliyoambiwa na wifi yake kama yana ukweli. Alishanga sana alipoingia jikoni. Alikuta kiloba cha kilo hamsini za sembe na mchele, mafuta ya kula lita kumi, sukari kilo tano, mkungu wa ndizi, pamoja na mahitaji mengine ambato nilikuwa nimewapelekea. Wifi yake alikiri kuwa hatamwamini tena wifi yake.

Baada ya siku kadhaa kupita alikuja binti yangu kuniita niende nyumbani ana mazungumzo na mimi. Nilipo nyumbani  binti yangu alitoka chumbani kwake akiwa na kifushi cha nguo. Alipiga magoti akiwa na maana ya kuniomba msamaha kwa niaba ya wenzake, kwa kuwa yaliyo pita ni ndwele, sikuona sababu ya kuhifadhi kinyongo nikiwa kama mzazi. Kwani mtoto akikunyea kwenye kiganja huwezi kukikata. Niliwasamehe kwani hawakufanya kwa maamuzi yao, bali kulikuwa ni shinikizo la mama. 

Ndani ya wiki hiyo, baba yangu alifariki. Nikiwa njiani kueleke nyumbani Nyambiti niliwasiliana na kaka yangu aliyekuwa hapo Dodoma. Tulionana na kuishia kusalillimiana tu. Kaka yangu ndiye aliyetoa hela ikiwa kama ubani. Lakini hiyo ilikuwa kana kisasi  alipizo kwamba alipofariki mkwe yaani mama yake sikwenda msibani. Hali kadhalika alipo faruki baba mkwe, mimi nilibaki na watoto kambini. Haikuwa rahisi kusafiri na familia nzima. Bali niliweka nguvu kwake pamoja na wadogo zake.


Lakini alikuwa amesahau kuwa wakati anafariki 

.















ACHA ABAKI KUWA MAMA.

Maad tangu uchanga wake, aluonekana ni mpole, sio msumbufu. Alipofikia umri wa miaka mitatu na kuendelea , alikuwa hapendelei kuongea. Alikuwa ni mkimya na hakupenda kucheza na wenzake. Hivyo waliomzidi umri na waliokuwa sawa kwa umri kwao ilikuwa ni nafasi nzuri ya kila baya kumsingizia na kumpa kipigo Maad.

Hajuwa kipenzi kwa mama yake mzazi kama walivyo watoto wenziwe. Kila mara na kila wakati mama yake alikuwa anamlalamikia kwa huli na lile pamoja na kumsemea kauli zisizo stahili kwake. Aliwahi hata kumwambia kuwa, ni mtoto gani yeye anayehangaika utadhani msukule. Hakukosa jina la kupewa kila uchapo.

Ulitokea wizi katika kambi niliyokuwa naishi. Maad alikuwa ni mmoja wa watuhumiwa. Lakini mambo tuliyamaliza kifamilia kuwa afisa aliyeibiwa hiyo Main Switch afidiwe kununua nyingine.

Kwa mtazami wa mama, Maad alionekana kuwa hafai tena kuishi ndani ya familia yake. Aliamua kumuondoa kumpeleka kwa mjomba wake mkoani. Maad kipindi hicho alikuwa ameisha anza kidato cha kwanza katika shule binafsi ya kulipia.

Kitendo cha wizi alifanya kusingiziwa tu, hata hivyo nilikata shauri la kusamehe ubaya aliopakazwa. Mkoani alianza masomo hadi alipo maliza kidato cha nne. Lakini mama yake hakutaka kabisa kumsaidia chochote kuhusu matumizi ya hapo shuleni, kila kitu niligharamia mwenyewe. Miaka yote minne hakuwahi kurudi nyumbani.

Maad alirudi nyumbani, wakati hio nilikuwa nimeisha farakana na mama yake kuhusu mambo ya ushirikina. Maad alifanikiwa kuchukua masoo ya Komputa, Lakini hakufanikiwa kupata ajira pamoja mama yake yake alikuwa ni afisa ajira kwenye kampuni kubwa la umma.

Nilimpigia kifua Maad akapata ajira katika vyombo vyetu vya usalama. Baada ya mafunzo alichaguliwa katika kazi maalumu katika moja mikoa yetu. Alishawishiwa na wenzake wakaangalie mwenendo mzima wa maisha yao kupitia sayansi mbadala.

Maad alipewa historia nzima utafikiri ama utadhania kuwa huyo mtoa historia alikuwepo. Kutokuwa kipenzi kwa mama yote ilikuwa ni njia ya kupitia. Kwa ufupi alikuwa afanywe kileta uchumi ndani ya maisha yake.