KATIBA
YA
MSIKITI
MASJID AL JIHADY
S.L.B. 8277 DAR ES SALAAM
Tafsiri ya maneno yaliyomo ndani ya muongozo wa Katiba hii ni kama ifuatavyo:-
1. Dini: Ina maana ya Uislamu kwa mujibu wa Qur an na suna za Mtume s.a.w.
2. Katiba: Ni muongozo na taratibu zitakazowekwa katika kusimamia shughuli zinazohusu Msikiti.
3. Msikiti: Ni Masjid Al Jihady Mpakani.
4. Madrasa: Ni Madrasa Al Jihady iliyo chini ya uongozi wa Msikiti.
5. BAKWATA: Baraza Kuu la Waislamu Tanzania ni mtoa hati ya utambulisho na mlezi wa Msikiti.
6. BAKWATA KATA: Baraza Kuu la Waislamu Tanzania ngazi ya Kata.
7. BAKWATA WILAYA: Baraza Kuu la Waislamu Tanzania ngazi ya Wilaya.
8. BAKWATA MKOA: Baraza Kuu la Waislamu Tanzania ngazi ya Mkoa.
9. Halmashauri ya Msikiti: Ina maana Bodi ya Wadhamini ambao ni waasisi wa Msikiti na viongozi wa Msikiti.
10. Muumini: Ni Muislamu anayehudhuria ibada za kila siku Msikitini.
11. Imam: Ni kiongozi mkuu katika shughuli za ibada.
12. Muislamu: Ni mtu yeyote aliye Muislamu anayeishi jirani kuuzunguka Masjid Al Jihady.
SEHEMU YA KWANZA
UTANGULIZI NA TAMKO.
Sisi waumini wa Kiislamu tunaosali katika Msikiti, na tulio jirani na MASJID AL JIHADY, uliopo mtaa wa Mpakani, Kata ya Kwembe, Wilaya ya Ubungo na mkoa wa Dar es Salaam; kwa pamoja tumekubaliana kuwa, muongozo huu ndio tutautumia kujiendesha, kuendesha msikiti na madrasa katika uboreshaji wa huduma mbalimbali za Msikiti na Madrasa.
Aidha muongozo huu utamuhusu muumini yeyote atakayeanza kusali na aliye jirani na MASJID AL JIHADY. Pamoja na hayo ifahamike kuwa Katiba hii siyo Qur an Tukufu. Hivyo basi Baraza la Wadhamini (Halmashauri ya Msikiti) inaweza kufanya mabadiriko yoyote kwa ushauri wa waumini, au itakavyoona inafaa kwa ajili ya ulinzi wa maslahi ya Uislamu na Waislamu kwa jumla.
SEHEMU YA PILI (2).
JINA NA ANUANI.
Ibara ya kwanza:
01. Jina la Msikiti.
Jina la Msikiti ni MASJID AL JIHADY.
02. Anuani ya Msikiti.
Anuani ya mskiti ni Kiwanja namba....Mtaa kwa Mpakani, Kata ya Kwembe, Wilaya ya Ubungo. S.L.B. 8277 DAR ES SALAAM.
SEHEMU YA TATU (3).
MALENGO, MADHUMUNI, DIRA NA DHAMIRA.
Ibara ya Pili:
01. Malengo na Madhumuni.
Malengo na madhumuni ya MASJID AL JIHADY ni kama ifuatavyo:-
(i). Kutekeleza ibada zote za dini, sherehe na sala ndani na nje ya mskiti.
(ii). Kusimamia, kufuatilia na kutoa mafunzo kwa Waislamu, na masomo mengine ya Kiislamu ya Kilimwengu ndani ya Qur an Tukufu, na suna za kipenzi cha Allah Mtume Muhammad s.a.w.
(iii).Kupokea au kutoa ruzuku, michango, misaada na zaka, kutoka au kwenda kwenye shirika, serikali au mtu binafsi ndani na nje ya nchi.
(iv). Kushirikiana na taasisi nyingine za kiislamu, serikali na misikiti inayo tambuliwa na serikali katika kupashana habari mbalimbali, zinazohusu uislamu kwa lengo la kuleta na kuimarisha maendeleo, umoja na amani katika nchi.
(v). Kuhamasisha jamii ya Kiislamu kuchangia shughuli za maendeleo ya Dini.
(vi). Kuboresha majengo ya Msikiti na Madrasa, kwa ajili ya kuwawezesha waumini na Waislamu kujifunza dini yao katika mazingira mazuri.
(vii). Kuwa na haki ya kupata, au kumiliki mali zisizo hamishika na zinazo hamishika, zinazo ambatana, zinazo tosheleza na zinazo hitajika kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa vitu vilivyo ainishwa hapo juu, au chochote kati ya hizo.
02. Dira ya MASJID AL JIHADY.
Kuwa ni taasisi ya mfano itakayo changia maendeleo endelevu ya jamii katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kijamii, kiafya, kielimu ya dunia na akhera kwa kuzingatia misingi ya dini ya Kiislamu.
03. Dhamira ya MASJID AL JIHADY.
(i). Kuwa ni taasisi yenye kutatua changamoto za jamii, ikiwemo elimu ya dini, ili iweze kuimarisha na kuimarika kiroho na elimu dunia. Pamoja na kuwapatia misaada ya kiutu kupitia mafungu ya zaka na sadaka nk.
Ibara ya Tatu:
01. Ulinzi na udhibiti wa Masjid Al Jihady.
Masjid na Madrasa Al Jihady kwa pamoja ni taasisi ya kisheria, itakayokuwa na uwezo wa kushitaki au kushitakiwa kwa misingi ya dini ya Kiislamu kupitia mamlaka ya Kiislamu inayo tambulika na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha MASJID AL JIHADY ikiwa ni taasisi, itakuwa chini ya umiliki wa Baraza la Halmashauri la Msikiti (Bodi ya Wadhamini) ambao ni waasisi na viongozi wa Mskiti.
SEHEMU YA NNE (4).
MUUNDO WA UONGOZI WA MSIKITI.
Ibara ya Nne:
01. Muundo wa Msikiti.
Kutakuwa na muundo wa uongozi katika MASJID AL JIHADY kama ifuatavyo:-
(i). Kutakuwa na baraza la Halmashauri ya Msikiti (Bodi ya Wadhamini).
(ii) Kamati Kuu
(iii). Idara ya Maendeleo
(iv). Waumini na Waislamu.
Ibara ya Tano:
Wajumbe na kazi za Bodi ya Wadhamini.
01. Wajumbe. Bodi ya wadhamini itakuwa na wajumbe wasiozidi kumi na moja (11), na wasiopungua wajumbe watano (5) tu, na itakuwa na wajumbe wafuatao:-
(i). Mwenye kiti wa Bodi.
(ii). Waasisi wa Msikiti watatu (3).
(iii). Wazee wa Msikiti wawili (2).
(iv). Muumini mmoja (1).
02. Kazi za Bodi ya Wadhamini.
Kazi za Wadhamini hizi zifuatazo:-
(i). Itafanya vikao vyake kila baada ya miezi mitatu, ili kipokea taarifa ya utendaji ya Kamati Kuu.
(ii). Kupokea, kujadiliana na kuthibitisha taarifa ya mapato na matumizi ya fedha na shughuli zote kutoka Kamati Kuu.
(iii). Kuhakikisha uendelezaji na utunzaji wa Msikiti na mali zake, na zingine ambazo zitapokelewa kama WAQFU. Pamoja na mali zinazo hamishika na ambazo hazihamishiki, zilizopo sasa na za baadae.
(vi). Itasimamia uchaguzi wa viongozi wa Msikiti kila baada ya miaka mitatu.
(v). Kufanya marekebisho ya Katiba.
(vi). Kupitia, kuchambua na kuidhinisha maandiko mbalimbali ya maendeleo itakayosimamiwa na MASJID AL JIHADY.
(vii). Kupitisha sera mbalimbali za uendeshaji wa taasisi kama itakavyoamriwa na wataalamu mbalimbali kwa misingi ya dini ya Kiislamu.
(viii). Kuidhamini taasisi katika shughuli zote zinazohusu Uislamu.
(ix). Kuona kuwa mambo ya Msikiti yanaendeshwa na Kamati Kuu kwa uangalizi wa Bodi ya Wadhamini.
(x). Bodi ya Wadhamini ndiyo yenye dhamana ya mali, na ni mmiliki wa Msikiti na Madrasa Al Jihady. Aidha itateua mkaguzi wa hesabu anaye tambulika na mamlaka ya Ukaguzi Tanzania kila baada ya miaka miwili.
Ibara ya sita:
Wajumbe na kazi za Kamati Kuu
01. Wajumbe.
Kamati Kuu itakuwa na wajumbe wasiozidi kumi na mbili (12) na wasiopungua saba (7) ambao ni;
(i). Mwenyekiti wa Msikiti.
(ii). Mwenyekiti Msikiti msaidizi.
(iii). Mweka Hazina.
(iv). Katibu Mkuu wa Msikiti
(v). Katibu Mkuu wa Msikiti msaidizi.
(vi). Imam Mkuu wa Msikiti.
(vii). Imam Mkuu wa Msikiti msaidizi.
(viii). Mwakilishi mmoja wa Idara ya Msikiti.
02. Kazi za Kamati Kuu ya Msikiti.
Kazi ama majukumu ya Kamati Kuu ya Msikiti ni haya yafuatayo:-
(i). Itashughulikia kazi za kila siku za MASJID AL JIHADY pamoja na Madrasa Al Jihady.
(ii). Itakusanya michango yote pamoja na mapato mingine ya kila siku kwa usimamizi wa mweka hazina kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini, na kuhakikisha kuwa hesabu sahihi na vitabu vya hesabu vinatunzwa.
(iii). Kuunda idara ya uendeshaji, kusimamia na kufuatilia mwenendo wa Msikiti na Madrasa. Pamoja na kupendekeza, kuteua, kuajiri, kuwasimamisha watendaji wake wa idara hizo kwa idhini ya Bodi ya Wadhamini.
(iv). Kuandaa mikakati ya kujenga uwezo wa wanajamii katika kutambua wajibu wao katika kujiletea maendeleo kwa misingi ya dini ya Kiislamu.
(v). Kutekeleza na kufuatilia maazimio ya waumini, kumchukulia hatua inayositahili muumini atakayefanya jambo kinyume na utaratibu uliowekwa, au atakaye kiuka maadili kwa mujibu wa katiba hii. Au kuupotosha umma wa Kiislamu wa eneo la Masjid Al Jihady kwa makusudi.
(vi). Kuteua na kuwaajiri Maimam, walimu wa Madrasa, au watendaji wengine kwa shughuli mbalimbali za Msikiti, na Madrasa Al Jihady kwa makubaliano maalumu, na kuidhinishwa na na Bodi ya wadhamini.
(vii). Kubuni mikakati ya uhamasishaji kwa jamii juu ya umuhimu wa kusoma Qur an, na kufanya ibada na suna kwa vitendo.
(viii). Kufanya matumizi halali kwa mujibu wa mahitaji ya Msikiti.
(ix). Kuunda kamati ndogo ndogo kulingana na mahitaji ya wakati ili kurahisisha utendaji kazi.
(x). Kamati Kuu itakaa kila siku ya Ijumaa au wakati wowote itakapo hitajika kulingana na mahitaji.
(xi). Itamchukulia hatua Muumini atakayekiuka kwa makusudi maadili kwa mujibu wa Katiba hii au kuupotosha Umma wa Kiislamu wa eneo la MASJID AL JIHADY.
(xii). Kuhakikisha kuwa taarifa za hesabu za mwaka zinatayarishwa, kuangaliwa na kuwasilishwa mbele ya Bodi ya Wadhamini kabla ya kuwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka.
(xiii.). Kila mwisho wa mwaka, Kamati Kuu itaandaa taarifa za utekelezaji wa majukumu ambayo yatafanyiwa uhakiki na yatawasilishwa katika Baraza la Halmashauri ya Msikiti.
SEHEMU YA TANO (5).
SIFA ZA WAJUMBE BODI YA WADHAMINI NA KAMATI KUU.
Ibara ya saba:
01. Sifa za Bodi ya Wadhamini.
Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini watatakiwa wawe na sifa zifuatazo:-
(i). Awe na elimu katika nafasi atakayoshika, awe na umri wa au zaidi ya miaka therathini.
(ii). Awe ni mkazi wa eneo la MASJID AL JIHADY na awe mwenye akili timamu.
(iii). Awe ni muumini anayehudhuria ibada za kila siku, mwenye kujitolea, sifa zinazoaminika kwa mujibu wa dini ya Kiislamu kama ilivyoagizwa ndani ya Qur an.
(iv). Awe mwadilifu, mbora wa tabia unaoheshimika katika kuhamasisha heshima ya Waislamu wenzao.
(v). Awe tayari kufuata utaratibu uliopo kwenye Bodi ya Wadhamini ya Msikiti, katika kuendesha shughuli za Msikiti/Madrasa na ibada.
(vi). Ngazi ya Imam Mkuu ni lazima awe na elimu ya dini ya Kiislamu, Qur an, suna na taratibu zingine zinazokubalika kwa misingi ya dini ya Kiislamu.
(vii).Imam Msaidizi atatokana na waumini ambao ni wakazi wenye kujitegemea katika eneo la Masjid Al Jihady kwa ushauri wa Imam Mkuu.
(viii).Kwa nafasi ya mwalimu wa Madrasa, sharti awe tayari kuwajibika kwenye Kamati Kuu.
02. Sifa za Kamati Kuu.
Wajumbe wa Kamati Kuu watatakiwa wawe na sifa zilizopo katika ibara ya saba (i), (ii), (iii), (iv) na (v)- 01 ya sifa za Bodi ya Wadhamini.
SEHEMU YA SITA (6).
KUPATIKANA KWA VIONGOZI BODI YA WADHAMINI NA KAMATI KUU.
Ibara ya Nane:
01. Kupatikana kwa viongozi.
Wajumbe/viongozi wa Bodi ya Wadhamini na Kamati Kuu, watachaguliwa kutoka miongoni mwa waumini katika mkutano Mkuu wa kawaida wa mwaka, ambao utafanyika mara moja kwa kila baada ya kipindi cha miaka mitatu.
SEHEMU YA SABA (7).
WAJIBU/MAJUKUMU YA VIONGOZI.
Ibara ya Tisa:
01. Mwenye Kiti.
Mwenye Kiti atakuwa na majukumu ama wajibu wa mambo yafuatayo:-
(i). Atakuwa kiongozi mkuu katika masuala ya kiutawala wa Msikiti na Madrasa, pamoja na mazingira yanayohusu taasisi hii.
(ii). Atakuwa msemaji wa Baraza la Wadhamini na mwangalizi mkuu.
(iii). Atawasilisha taarifa kwenye mkutano mkuu kuhusu sera ya Bodi ya Wadhamini.
(iv). Ataongoza mikutano yote na kusimamia shughuli za msikiti, au kwa kupitia wakuu wa idara za maendeleo ya msikiti.
(v). Atakuwa ni mmoja wa watia saini katika akaunti na nyaraka zote, pamoja na kuidhinisha hati za malipo ya fedha, hundi, au malipo yoyote.
(iv) Atakuwa na mamlaka ya maamuzi yoyote yahusuyo shughuli za msikiti, na uongozi mzima wa kamati kuu, pale inapolazimu kufanya hivyo.
(v). Mwenye Kiti msaidizi atatekeleza haya yote kwa niaba ya Mwenye Kiti.
02. Mweka Hazina.
Mweka Hazina atakuwa na majukumu ama wajibu wa yafuatayo:-
(i). Atatunza kumbukumbu za fedha.
(ii). Ataandaa hati zote za malipo, na atadhibiti fedha za Bodi kwa usimamizi imara.
(iii). Atapokea na kukusanya michango na sadaka mbalimbali toka kwa wahisani na Waislamu wa ndani na nje ya Kata ya Kwembe.
(iv). Ataandaa na kutoa taarifa ya fedha kila robo, nusu, robo tatu ya mwaka na mwaka katika Baraza la Halmashauri ya Msikiti na mikutano ya Kamati Kuu.
(v). Ataandaa taarifa ya mizania kwa madhumuni ya ukaguzi inapobidi.
(vi). Atakuwa ni mmoja wa watia saini katika akaunti ya Msikiti.
03. Katibu Mkuu.
Katibu Mkuu atakuwa na majukumu ama wajibu wa yafuatayo:-
(i). Ataitisha mikutano yote kwa kushirikiana na Mwenye Kiti.
(ii). Ataandaa agenda za vikao na mikutano na kuchukua taarifa/dondoo wakati wa vikao na mikutano.
(iii). Ataandaa nyaraka za Msikiti, atazitunza na atazisambaza kwa utaratibu maalumu. Pia atatuma taarifa za mali zote zinazohamishika na zisizohamishika.
(iv). Atakuwa mtendaji mkuu wa shughuli za Msikiti na Madrasa au kwa kuwakilishwa na mkuu wa idara husika.
(v). Atakuwa ni mmoja wa watia saini katika akaunti ya Msikiti.
(vi). Atasimamia, atatetea na kufuatilia haki za waumini/Waislamu; waliopatwa na changamoto au matatizo yanayohitaji msaada, akishirikiana na wataalamu wengine kulingana na matatizo yalivyo.
(vi)Atakuwa Katibu wa Bodi ya Wadhamini na atawajibika kwa Mwenye Kiti wa Kamati Kuu.
04. Imam Mkuu.
Imam Mkuu atakuwa na majukumu ama wajibu ya yafuatayo:-
(i). Atakuwa Kiongozi Mkuu, mwenye tamko la mwisho kwa masuala ya shughuli zote za kidini na ibada, ndani ya maeneo ya Masjid na Madrasa Al Jihady pamoja na shughuli za ndoa, maulid, hitima, vifo, kutangaza muandamo wa mwezi, na maelekezo mengine ya kiimani kwa mujibu wa Qur an na Suna za Mtume s.a.w. pamoja na maelekezo kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
(ii). Atakuwa ni mmoja wa watia saini katika akaunti ya Msikiti.
(iii). Atasimamia shughuli zote za
Msikiti au kwa kupitia Wakuu wa idara za Maendeleo ya Msikiti.
(iv). Atawajibika kwa Mwenye Kiti wa Bodi ya Wadhamini.
(v). Iwapo Imam Mkuu atakuwa na dharura, Imam Mkuu msaidizi atamuwakilisha katika shughuli za ndani na nje ya Msikiti. Lakini iwapo Imam Mkuu Msaidizi naye atakuwa na dharura, Mwenye Kiti atamchagua mjumbe mmoja kutoka Kamati Kuu kukaimu nafasi ya Imam Mkuu katika kikao hicho.
(vi). Atakuwa msemaji Mkuu wa masuala ya dini na taasisi.
SEHEMU YA NANE (8).
KUCHAGULIWA/KUTEULIWA TENA KATIKA UONGOZI.
Ibara ya Kumi:
01. Uchaguzi.
Uchaguzi wa viongozi kwa mara zaidi ya moja itakuwa ifuatavyo:-
(i). Kiongozi wa ngazi yoyote anayo haki ya kuchaguliwa kwa mara nyingine tena baada ya muda wake wa awali kumalizika.
02. Kuteuliwa.
Uongozi wa kuteuliwa utakuwa kama ifuatavyo:-
(i). Pengo la nafasi ya uongozi linapotokea, nafasi hiyo itajazwa na Kamati Kuu na kuwataarifu wajumbe wa Bodi ya Wadhamini na Waumini.
SEHEMU YA TISA (9).
KUKASIMU MÀDARAKA YA BODI YA WADHAMINI.
Ibara ya kumi na moja:
01. Kukasimu Madaraka.
Bodi ya Wadhamini wa Msikiti na Madrasa, wakati wowote na sababu yoyote ile, inaweza kukasimu madaraka yake kwa Kamati Kuu, ili kufanya shughuli zake muhimu na kutoa maamuzi ya utendaji ili kufanikisha malengo ya taasisi.
SEHEMU YA KUMI (10).
SHUGHULI ZA KIFEDHA, BENKI NA AKAUNTI.
Ibara ya kumi na mbili:
01. Fedha na Benki.
Kutakuwa na mambo yafuatayo:-
(i). Itafunguliwa akaunti ya fedha kwa kutumia jina la MASJID AL JIHADY katika benki watakayo kubaliana Waumini, kupitia Kamati Kuu na Bodi ya Wadhamini katika mkutano wao.
(ii). Kati ya Mwenye Kiti, Katibu, Mweka Hazina na Imam Mkuu watahusika kufungua akaunti hiyo.
(iii). Watu wawili kati ya waliofungua akaunti hiyo, wataruhusiwa kutoa fedha kwenye akaunti.
(iv). Idhini ya kufungua akaunti hiyo itathibitishwa na muhitasari wa kikao cha Bodi, kwa orodha ya majina ya watakao husika na ufunguaji wa akaunti pamoja na vyeo vyao.
SEHEMU YA KUMI NA MOJA (11).
KANUNI ZA MAADILI KWA VIONGOZI NA WAUMINI.
Ibara ya kumi na tatu:
01. Kiongozi wa Msikiti/Madrasa.
Kiongozi yeyote wa Msikiti, Madrasa au katika moja ya idara za Msikiti lazima:-
(i). Awe mstari wa mbele kutetea masilahi ya Waislamu na mali za Msikiti na Madrasa, kufanya kazi kuzingatia misingi ya dini ya Kiislamu kwa kusimamia yafuatayo:-
(a). Haki na ukweli
(b). Uwazi na uaminifu
(c). Upendo na kujitolea.
(ii). Kiongozi yeyote atakaye kiuka maadili, kanuni na masharti ya muongozo wa Katiba hii, kukiuka misingi ya Kiislamu, itakapothibitishwa hivyo, ataachishwa uongozi mara moja kwa uwezo wa Kamati Kuu.
SEHEMU YA KUMI NA MBILI (12).
WAJIBU WAUMINI NA WAISLAMU WA MASJID AL JIHADY.
Ibara ya kumi na nne:
01. Wajibu wa waumini.
Waumini wa Kiislamu wa Masjid Al Jihady watakuwa na wajibu ufuatao:-
(i). Kushiriki katika ujenzi, uendelezaji na uboreshaji wa huduma za Msikiti na Madrasa kwa hali màli.
(ii). Kutoa taarifa kwa uongozi za waumini au Waislamu wageni wanaohamia katika maeneo jirani na msikiti.
(iii). Si ruhusa asiye kiongozi kufanya majukumu ya moja kwa moja ya uongozi bila idhini ya ama ruhusa ya uongozi.
(iv). Kila muumini anayo haki ya kupata taarifa za Msikiti/Madrasa, kushauri au kutoa maelekezo ya jambo lenye faida kwa Msikiti kwa kupitia vikao vya ndani ya Msikiti.
(v). Kila muumini au muislamu ana haki ya kutumia Msikiti au Madrasa au Mazingira yake kwa shughuli za kidini, kwa kutoa taarifa na kupewa ruhusa ya jambo hilo.
(vi). Kushiriki shughuli zitakazoagizwa na viongozi kwa maendeleo ya Msikiti na Madrasa.
(vii). Kufuata taratibu zote za ibada zilizowekwa na uongozi ndani ya Msikiti.
(viii). Kuendesha ibada kuanzia kusoma adhana, kukimu sala na kusalisha. Iwapo muda wa ibada umefika na hakuna Imam Mkuu wala msaidizi wake, au kiongozi yeyote wa Msikiti.
(ix). Muumini yeyote atasalisha kwa idhini ya Imam Mkuu au kiongozi.
(x). Atatoa sadaka na zaka kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Kiislamu.
SEHEMU YA KUMI NA TATU (13).
IDARA ZA MAENDELEO YA MSIKITI.
Ibara ya kumi na tano:
01. Idara za Maendeleo.
Kutakuwa na idara za maendeleo ya Msikiti zifuatazo:-
(a). Elimu ya dini (Madrasa).
(b). Zaka na Sadaka.
(c). Hijja na Umrah na
(d). Ujenzi na Mazingira.
SEHEMU YA KUMI NA NNE (14).
MKUTANO MKUU.
Ibara ya kumi na sita:
01. Mkutano Mkuu.
(a). Kutakuwa na mkutano mkuu wa kawaida wa mwaka, ambao utafanyika mara moja kwa mwaka ndani ya mwezi Desemba. Utahudhuriwa na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini, wajumbe wa Kamati Kuu na waumini wa Msikiti huo.
(b). Mkutano Mkuu wa kawaida wa mwaka utajadili yafuatayo:-
(i). Kufanya majadiliano ya kuidhinisha taarifa ya mwaka ya Mwenye Kiti.
(ii). Kujadili taarifa ya fedha ya mweka hazina.
(iii). Kujadili maendeleo ya Msikiti au mambo yoyote yatakayojitokeza.
(c). Kuteuwa wakaguzi wa hesabu wa nje pale inapobidi kwa ajili ya ukaguzi wa kina wa hesabu za Msikiti. Kuwateuwa watumishi, Wadhamini ambao mara kwa mara huonekana ni wa lazima kwa usimamizi mzuri wa Msikiti.
(d). Kutakuwa na mkutano Mkuu maalumu ambao utaitishwa wakati wowote kwa mwaka iwapo kutakuwa na mambo muhimu na hayawezi kuusubiri Mkutano Mkuu wa kawaida mwaka.
(e). Mkutano Mkuu wa kawaida/maalumu utafanyika tu iwapo idadi ya wahudhuriaji itafikia theruthi mbili (2/3) ya waumini wote wanohitajika.
SEHEMU YA KUMI NA TANO (15).
UKOMO WA VIONGOZI NGAZI ZOTE.
Ibara ya kumi na saba:
01. Ukomo wa viongozi.
Kiongozi wa ngazi zote atakoma kuwa kiongozi kutokana na:-
(i). Kifo
(ii). Kujiuzulu au kustaafu
(iii). Maradhi ya muda mrefu kuanzia miezi mitati (3) na kuendelea, ambayo hatakuwa na uwezo wa kutimiza majukumu ya Al Masjid Jihad kama kupatwa na ukichaa, wenda wazimu au kutokuwa na akili timamu nk.
(iv). Kufukuzwa au kukataliwa kwa idadi ya theruthi mbili (2/3) ya waumini.
(v). Kutohudhuria vikao kwa muda wa miezi miwili mfurulizo bila sababu maalumu.
(vi). Kutohudhuria ibada za kila siku kwa muda wa miezi miwili mfurulizo bila sababu maalumu.
(vii). Kuhamia eneo jingine lisilo la Masjid Al Jihady.
(viii). Kutowajibika kwa nafasi ya uongozi aliyonayo kwa miezi miwili mfurulizo bila sababu maalumu.
SEHEMU YA KUMI NA SITA (16).
MABADIRIKO YA KATIBA NA UTATUZI WA MIGOGORO
Ibara ya kumi na nane:
01. Mabadiliko ya Katiba.
Ppm
Mabadiliko ya Katiba yatafanyika kwa utaratibu ufuatao:-
(i). Katiba itafanyiwa mabadiliko kwa maamuzi ya Bodi ya Wadhamini kwa theruthi mbili (2/3) ya wajumbe watakao shiriki katika mkutano ulioitishwa kwa ajili hiyo.
(ii). Mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba yatawasilishwa kwa Katibu Mkuu siku ishirini na moja (21) kabla ya mkutano husika.
(iii). Toleo jipya la Katiba litapelekwa BAKWATA na nakala nyingine zitapelekwa benki na sehemu zingine husika.
02. Utatuzi wa migogoro:
Migogoro yote itasuluhishwa chini ya ya:-
(i). Kamati Kuu ya Msikiti.
(ii). Baraza la Halmashauri (Bodi ya Wadhamini).
(iii). Ofisi ya BAKWATA Kata na Wilaya.
Iwapo itashindikana kupata suluhisho la migogoro katika hatua Ilizo tajwa hapo juu. Basi, migogoro itapekwa kwa mlezi Mkuu wa Msikiti BAKWATA Makao Makuu.
SEHEMU YA KUMI NA SABA (17).
HITIMISHO.
Katiba imepitishwa na Bodi ya Wadhamini wa Msikiti na kusainiwa na viongozi wakuu wafuatao:
............................. .................................
MWENYE KITI. KATIBU MKUU
BODI YA WADHAMINI.