Saturday, February 11, 2023

MFADHILI MBUZI.

MFADHILI MBUZI.


(Sehemu ya kwanza)

Nilikuwa na rafiki, alikuwa ni rafiki yangu hasa. Tulisaidiana kwa kila hali na kwa gharama ambazo tuliweza kuzikabiri.

Urafiki wetu ulidumu kwa muda mrefu sana. Baadhi ya familia iliyokuwa imetuzunguka walituchukulia kuwa sisi ni ndugu. Kwa upande wangu naweza kusema kuwa tulikuwa ndugu, kwani upendo tuliokuwa nao, ulikuwa ni wa hali ya juu kuwazidi hata walio zaliwa kwa mama na baba mmoja.

Rafiki yangu alikuwa ni mcheshi kupindukia, mimi mwenyewe sikumfikia. Alikuwa anajulikana kwa jina la 'Matatizo.' Hakuwa na matatizo yoyote bali alikuwa na ule ucheshi uliopelekea kuonekana kama vile ni  mtu mwenye matatizo. Lakini haikuwa hivyo, hata hivyo jina hilo walilifupisha na kumwita 'Tizo'.

Mimi rafiki yake jina langu kidogo lina historia yake kabla hata hatujawa marafiki. Wakati nilipokuwa katika shughuli zangu za kiusalama. Nilikuwa nakabiriana na mazingira ambayo yalikuwa hatarishi. Hivyo basi nilipofanikiwa katika kujikinga au kujiepusha na hali hiyo, nilitumia neno la kilugha 'mafujo gatufuja'.

Hii ilikuwa na maana kwamba mlenga au mlengwa shabaha au lengo lake limekosa mafanikio. Hivyo basi jamii iliyokuwa imenizunguka waliona ni jina refu kulitamka, wakalibatiza na kuwa jina la 'Fujo'.

Siku moja mimi na rafiki yangu tulikuwa mahali patulivu, tulikuwa katika mapumziko ya kawaida. Tulikuwa hatika hali ya kupeana ushauri, maoni na kupeana mawazo mbalimbali huku tukijiburudisha kwa kinywaji cha moja mbili baridi au moto, hii ilikuwa ni kawaida yetu baada ya kazi ya kutwa nzima.

Wakati tunaendelea na viburudisho ya vinywaji, rafiki yangu alikuwa na lake jambo, ambalo kwa siku hiyo alianza kunisimulia kwa undani zaidi. Nilimsikiliza kwa makini sana. Lakini wakati huo tayari tulikuwa tumechangamka kiasi fulani kwa kinywaji. Tuligonganisha viganja vyetu yaani ngumi, ikiwa kama ishara ya pendo na kuaminiana, kwa mazoea 'nipe tano', kisha alianza kuniambia:

"Ndugu yangu Fujo nakuomba unisikilize kwa makini halafu utanipa ushauri. Bila shaka marehemu shemeji yako ulikuwa unamfahamu vizuri sana. Kabla hatujawa na ndoa naye, wala kuwa na utambulisho kwa wazazi wake, kilitokea kifo cha baba yake mzazi."

"Baba yake alikuwa ni dereva wa magari makubwa yafanyayo safari za mikoani na nje ya nchi. Katika hali ya kuchoka na safari ndefu aliamua kuliegesha gari lake kwenye moja ya vituo vya mafuta mkoani Pwani. Nia yake ilikuwa apate muda kidogo wa kupumzika. Kwa mapenzi ya Mungu hakuweza kuamka tena, huo ukawa ndiyo mwisho wa uhai wake. Kweli uhai ni koroboi."


(Sehemu ya Pili)

Kama nilivyokujuza. Tizo alikuwa ni mcheshi sana, hata alipokuwa ananisimulia tukio hili, ukweli hakuweza kuonesha hali ya masikitiko wala mabadiriko yoyote. Bali alikuwa ni mtu wa vicheko vya hapa na pale muda wote. Niliitafakari sana simulizu hiyo ilikokuwa inaelekea na mwisho wake ni wapi. Pamoja na ubashiri wangu lakini nilishindwa kupata jibu la haraka nilimwacha aendelee kunisimulia:

"Unasikia bwana Fujo, baba huyo alikuwa na watoto wawili tu wakike, mmoja wapo ndiyo huyo marehemu mke wangu. Huyo baba aliwahi kuishi na mwanamke ambaye hakufanikiwa kupata mtoto."

Mwanamke huyo alikuwa na mdogo wake wa kike ambaye naye alikuwa na watoto watatu, wawili wa kike na mmoja wa kiume. Mwanamke huyo alikuwa ndio mlezi wa watoto wote hao."

"Hawa wawili waliokuwa wa huyu baba, wao walikuwa ni wakubwa wamefikia kuutambua usichana wao. Ila hawa wengine watatu wao walikuwa bado shule ya msingi."

Ni dhahiri maelezo ya simulizi hii yalinivutia, sikuwa na haja ya kuingilia kati mara kwa mara wakati rafiki yangu alipokuwa ananisimulia. Zaidi ilikuwa ni kasi ya kinywaji, ilikuwa inapanda na kushuka. Simulizi nayo ilikuwa inaleta taswira fulani hivi ya kifamilia. Nilimuuliza iwapo aliwahi kutoa msaada au kuhudhuria msiba wa huyo baba. Bwana 'Tizo' aliendelea kunijuza :

"Ndugu yangu Fujo, sikuweza kwenda, kwani wakati huo  penzi letu ndio kwanza lilikuwa kwenye gia namba moja. Kama nilivyosema hapo mwanzo, sikuwahi kutambulishwa popote. Niliwahi kuoneshwa picha tu na hata hao wengine pia. Ila nilimuwezesha mke wangu safari ya kwenda kwenye msiba wa baba yake na kurudi."

"Ilikuwa ni mtihani kwa mke wangu, kwani baada ya siku kadhaa ndani ya kifo cha baba yake, mke wangu alipokea taarifa za ungojwa wa mama yake mzazi, ambaye nae nilimuona kwenye picha tu.  Nilimsafirisha mke wangu kwenda kumuuguza mama yake. Lakini alipangalo Mungu binadamu hana ujuzi nalo. Mungu alimpenda zaidi. Mama naye alipoteza maisha. Mungu amsamehe dhambi yake na amuepushe na adhabu ya kaburi. Aamin."

Aisee inatia huruma sana, nilipata maswali kadhaa, kwa nini vifo vifuatane kwa muda mfupi hivyo? Tena ni kwa wazazi tu? Ingawa tulikuwa hali ya kuburudika, mhuu, ilikuwa inachoma, inauma kinoma kweli kweli. Hata hivyo muda wote nilikuwa najaribu kumsisitiza awe jasiri. Nilimuuliza kwa mara nyingine iwapo alibahatika kuhudhuria msiba wa mama mkwewe. Tizo alisogeza kiti na alijitengeneza na kukaa vizuri mithili ya Hakimu afanyavyo wakati wa kutoa hukumu, kisha alinijibu.

"Acha tu Bwana Fujo, rafiki yangu. Taarifa za msiba zilipotufikia kwa bahati nzuri wakati huo nilikuwa na safari ya mkoa jirani na kwenye msiba. hivyo nilifanikwa kufika msibani baada ya siku moja ya mazishi. Ila nilikuwa na masikitiko makubwa, mke wangu kuondokewa na wazazi kwa mpigo na kuwaacha kwa jina la 'watoto yatima au watoto wa marehemu."

"Nilipofika msibani mke wangu ndiye aliyenipokea na kuniongoza hadi kwa dada yake. Hapo ndipo nilipoweza kumuona dada yake mzaliwa wa tumbo moja na mke wangu kwa baba mmoja. Pia nilitambulishwa kwa huyo mama mkwe mlezi, pamoja na mama mkwe mdogo mlezi mwenye wale watoto watatu."

" Muda wa jioni ulipofika, tuliongozana na mke wangu hadi nyumba ya wageni iliyokuwa jirani na nyumbani kwa mama mkwe mlezi ambako tulichukua chumba. Baada ya siku tatu niliruhusiwa kuondoka na mke wangu kwa kuwa msiba ulikuwa umeisha kwa mujibu wa desturi na mila za kiafrika. Yaani kuinua tanga."

"Baada ya kuwa tumerudi  masikani petu, nilifanikiwa kumbadirisha marehemu mke wangu na kuwa katika muonekano mwingine wa maisha. Nilimpeleka shule ya ushonaji nguo, kisha nikimfungulia kituo cha ushonaji na biashara ya nafaka na vinywaji. Haya yote bwana Fujo niliyafanyaya kabla hata hatujafunga nae ndoa yetu."

"Tuliishi kwa amani na furaha tele. Ilifikia kipindi niliweza kumtambulisha mke wangu kwa baba yangu mzazi, ambaye aliniamuru nifunge ndoa mara moja, na niliitimiza amri hiyo. Baada ya hapo mke wangu alionekana ni kioo katika baadhi ya ndugu zake. Aliweza kuwasaidia pale alipoweza kwa fedha na hata vitu na mawazo pia. Baadhi ya ndugu walimtembelea kwenye makazi yake, naye alijaliwa kuwakarimu kwa kadri alivyo weza. Lakini, kuna msemo usemao 'chema hakidumu'. Yote ni mapenzi ya Mungu mwenye kuyajua tusiyoyajua."


(Sehemu ya Tatu).

Kauli hiyo ya rafiki yangu ilinishitua sana. Mengi nilijiuliza kimoyo moyo ni nini alichotaka kuongelea? Ni madhira gani tena yalimsibu? Pamoja yalikuwa yananichoma lakini ilibidi nimvumilie, sikuwa na jinsi. Lakini rafiki yangu alikuwa vizuri tu hakuwa na kigugumizi wala msito. Alikuwa anaongea kama mashine ya kukoboa mhindi.  Niliendelea kumsikiliza:

"Ilifika wakati mke wangu alishika uja uzito ambao haukuwa ni liziki, mimba iliharibika au kutoka ndani ya ukomavu wake. Lakini kwa mara nyingine tena, Mungu alimjalia kushika mimba, alijifungua mtoto wa kike kwa njia ya upasuaji. Nilimshukuru Mungu muumba wa mbigu na ardhi."

"Mtoto wetu alipopata umri wa miaka mitatu, tulimwanzisha shule ya awali au chekechea. Lakini maisha bwana Fujo ni sawa na maua. Mke wangu alianza kupata homa za hapa na pale, mara tumbo, yaani kila uchao ulikucha na ugonjwa mpya."

"Miradi yote ilisimama kwa ajili ya kumhagaikia afya yake, . Ilifika wakati hakuweza tena kufanya lolote, ngoma niliipiga na niliiicheza mwenyewe. Nilibaki mimi peke yangu muhudumiaji wa mgonjwa mke wangu kwa kila kitu. Ndugu yangu Fujo, yaone kwa mwenzio omba yasikukute. Aisifiye mvua fahamu imemnyeshea. Tulikuwa na dada msaidizi wa ndani nae alisepa. Acha tu, nilikuwa baba na ndiyo mama vile vile mtoto."

Nilifanya kama kumkatiza mazungumzo yake, kwani nilihitaji kufahamu iwapo aliomba msaada kutoka ukweni kwake ikashindikana. Je, kwa ndugu zake yeye mwenyewe? Hata hivyo alinijibu:

"Weee acha tu uitwe Fujo na mimi Tizo. Ni majina yenye herufi nne nne tu. Msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Msaada niliupata kutoka ukweni kwangu. Bahati kilikuwa ni kipindi cha likizo ya wanafunzi. Mama mkwe mlezi alimtuma shemeji yangu ambaye alikuwa kamaliza kidato cha nne, hivyo alikuwa anasubiri matokeo mtihani. Tulimpokea na tulimshukuru mama mkwe mlezi."

"Baada ya siku kadhaa kupita, matokeo ya kidato cha tano yalitoka shemeji yangu akiwa mmoja wao wa washindi. Hivyo ilimbidi arudi nyumbani kujiandaa kwenda kidato cha tano."

"Kipindi hicho mgonjwa alionekana na alinipa matumaini makubwa, kwani alianza kuimarika na kurudi katika hali yake ya kawaida. Madaktari nao walituthibitishia kuwa mgonjwa anaendelea vizuri, bali atumie lishe bora pamoja na dawa."

"Mke wangu aliniomba aende kwao ili anipumzishe na pilikapilila za gumuuguza. Sikuona sababu ya kumkatalia. Nilimsafirisha hadi kwao kwa mama mkwe mlezi. Huwezi kuamini mshikaji wangu, tumwachie Mungu mwenyewe, kwani alikuwa na makusudio yake ambayo binadamu hawezi kuyabaini."

"Baada ya siku kadhaa kupita, mama mkwe mlezi alinipigia simu, alinifahamisha kuwa mke wangu hali yake siyo nzuri. Hivyo wapo hospitali kuu ya mkoa. Alinihimiza nimtumie vyeti alivyokuwa anavitumia huku kwa matibabu kwani vinatakiwa. Sikufanya ajizi, nilijitahidi na nilifakiwa kuvituma vyeti hivyo kwa wakati. Lakini kila uchao nilipewa taarifa ya mgonjwa kuzidiwa."

(Sehemu ya Nne)

Ingawa maelezo ya rafiki yangu yalikuwa yananichoma, lakini sikuwa na la kufanya, bali nilitumia muda wangu wote kumpoza kwa kumpa pole. Hata hivyo rafiki yangu alikuwa ngunguli badala ya kuwa ngangali. Alikuwa hana wasiwasi wala dalili zilizomuonesha kuhuzunika wala kusikitika ila aliendelea kunieleza:

"Nilipopata taarifa za kuzidiwa kwa mke wangu, nilifunga safari ya kumfuata huko aliko. Niliondoka na dawa za tahadhali alizokuwa anazitumia. Nilimkuta kweli ana hali mbaya. Nilimhudumia kwa dawa nilizo kwenda nazo; baada ya siku mbili alipata unafuu fulani ambao aliweza kula na kunywa maji na maziwa kidogo."

"Sikuona sababu ya kurudi nae, kwani pale palikuwepo watu wa kumhudumia. Niliamua kwenda kituo cha usafiri kupata tiketi ya kurudi masikani kwangu. Wakati nilipokuwa hatua chache kuingia eneo la kituo hicho, nilipokea simu iliyotoka kwa shemeji yangu msomi wa kidato cha tano. Aliniambia nisikate tiketi, kwanza nirudi mama mkwe mlezi kaagiza.

"Nilijiuliza, kimetokea nini nyuma yangu? Nilipata hofu kuhusu mgonjwa wangu labda hali yake imebadilika tena. Nilifanya haraka kurudi kwa mwendo wa one 'twenty'. Nilimkuta shemeji yangu nje anafua nguo zake. Nilipoingia ndani nilimkuta mama mkwe mlezi anaongea na mwanamke mwingine aliye dai kuwa ni nduguye. Mezani kulikuwa na lita ya pombe 'kimpumu'."

"Bila aibu, mama mkwe mlezi aliniambia kuwa hawezi kubaki na mgonjwa kutokana na maneno yanayozungumzwa na baadhi ya ndugu. Hata shemeji yangu nae alikataa kata kata kwamba iwapo mama yake amekataa yeye hana mamlaka tena. Alinijibu bila hata kuniangalia usoni."

"Bwana Fujo, kua uyaone ya dunia. Ghafla macho yangu yalipata ukungu, rangi saba za dunia ziliangaza machoni pangu. Bila kusita nilichukua maamuzi magumu. Niliamua kuondoka nae mke wangu pamoja na mtoto wetu. Mama mkwe mlezi alishangilia kwa kupiga makofi pamoja na mwanamke aliyekuwa naye. Walicheka kicheko cha kufurahia huku wakisindikiza furaha yao kwa kimpumu."

"Kesho yake wakati tunaondoka na washirika wangu, yule mama alitoa kilio kilichokuwa na kauli ya eti kashindwa kumuuguza mwanae. Kitendo hicho kilinisikitisha sana. Lakini Mungu ni mwema. Nilisafiri na mgonjwa wangu bila usumbufu wowote hadi masikani kwetu."

"Nilimuanzisha tiba mara moja. Lakini ndani ya miezi miwili ya tiba yake, mke wangu alipoteza maisha. Mwenyezi Mungu ampe kauli thabiti. Aamin."

"Niliwaza mengi kuhusu kifo cha mke wangu. Nilijumuisha matukio yote ambayo yalinisononesha sana. Bwana Fujo, kama ni dhambi namuomba Mungu anisamehe. Lakini siyo bure kulikuwa ma jambo lao zima."

Ilikuwa ni kazi kweli kweli, nilimsihi rafiki yangu kwamba yote amshitakie Molla wetu ambaye ni mjuzi wa kila jambo. Tena tusiache kumuombea dua pamoja na wengine waliotutangulia mbele ya haki. Mungu awaondoshee dhambi zao. Nilitaka kufahamu iwapo ndugu wa upande wa ukweni walifika kwenye msiba wa mke wake. Alinijibu:

"Ndugu yangu Fujo, ni mama mkwe mlezi tu ndiye aliyefika, wengine hawakuonekana. Halafu mama huyo alijitoa ufahamu eti alimfuata mjukuu akamlee. Lakini nilipo kumbuka ya nyuma, nilikataa laa hasha sihitaji msaada wowote kutoka kwao. Pamoja na kwamba mke wangu nilimchukua kutoka mikoni mwake. Lakini baada ya muda kupita niliwasamehe. Nilifika masikani kwao kwa nia ya kujenga upendo na undugu."

"Mara ya mwisho niliwatembelea ukweni nikiwa tayari nimeisha oa mke mwingine ambaye ni huyu niliye nae sasa. Hatua hii ilifungua ukurasa mpya. Wakati huo shemeji yangu alikuwa Chuo cha Uwalimu. Likizo zake zote alipumzika nyumbani kwangu. Nilimuhudumia kadri nilivyoweza. Udada na mke wangu ulipamba moto. Ilikuwa sio rahisi kuwapambanua tabaka za undugu wao."

"Shemeji yangu alipomaliza chuo aliishi nyumbani kwangu akiwa na subira ya ajira. Nilimsaidia katika utafutaji wa kazi na hata katika utaratibu wa uandishi wa barua za maombi ya kazi."


(Sehemu ya Tano)


Rafiki yangu alizidi kuwa kausha mate kwa kuongea, ila nilimsifu kwa uvumilivu wake. Haya yangekuwa yametokea kwangu mimi, hapana, hapana kabisa. Yaani hata huyo shemeji yake hakuwa na aibu kwenda kuishi mahali ambapo alikataa kumuuguza. Lakini kitendo cha rafiki hangu kuwasamehe, basi wao wangemshika bega kama sio sikio. Palikuwa na ukimya fulani wa shetani kapita. Ndipo alipoendelea kunijuza zaidi:

"Siku baada ya siku, shemeji yangu alihamia mbali na kwangu aliko dai kuwa ni kwa mama yake mdogo mwenye kituo cha ususi nakadhalila, hivyo basi alikuwa anachukua ujuzi ili ajikumu na maisha. Huyo mama yake mdogo sikuwahi kumuona."

"Haukupita muda, alihamia aliko dai kuwa ni kwa mjomba wake, ambaye nae sikuwahi kumuona. Mara ya mwisho alimtuma mti amchukulie nguo zake zilizokuwa hapa nyumbani kwangu. Siku iliyofuata nilipata taarifa kuwa amesafiri kurudi kwao. Hazikupita siku nyingi, nilipewa taarifa kuwa amejifungua mtoto wa kike."

"Nilitafakari, kwa nini shemeji yangu alipokuwa hapa kwangu, aliniomba nisimwambie mama mkwe mlezi kuwa yeye yupo hapa kwangu? Alikuwa na lengo gani?"

"Kipindi alichomuuguza mke wangu, kwa nini hakuwahi kumzungumzia mama mdogo wala mjoba wake? Lakini ndugu yangu, mtu atakunyima chakula na sio neno. Shemeji yangu alikuwa na lake jambo. Sijui kama kulikuwa na wengine nyuma ya pazia wakiwa na lao moja."

"Shemeji yangu alipokuwa huko kwao alikuwa anawasiliana na shoga yake kwamba, eti huyu mke wangu wa sasa yupo hapa kuponda mali tu. Pili, hataki kunizalia watoto, kila anaposhika mimba anazitoa. Tatu, mimi na mke wangu tunamdhurumu mtoto wa marehemu mali zake. Tumeuza viwanja na gari ambavyo ni mali ya mtoto. Nne, nyumba tunayoishi haina mabadiliko yoyote, hata vitu vya ndani pamoja na kitanda tunacho lalia ni kile kilichoachwa na dada yake marehemu."

"Bahati mbaya na nzuri, wakati wa mawasiliano yao, kulikuwa na mtu mwingine kati yao ambaye ni damu damu na mke wangu. Habari hizi zilipo mfikia mke wangu, alimpigia simu shemeji yangu kufahamu ukweli. Lakini alikana kata kata na alimtupia mpira huo shoga yake.

" Uzuri ni kwamba wakati wa mahojiano shoga yake alikuwapo pia simu ilikuwa na sauti ya nje kila kitu kilisikika. Nilimtuma mama mmoja ambaye wanafahamiana na mama mkwe mlezi kwamba, awasiliane nae kutaka kupata ukweli. Lakini mama yule kabla maongezi hayajafika mwisho, simu yake ilikatika. Tangu hapo hakupatikana tena, na alipopatikana hakupokea simu, na hata huyo shemeji yangu pia."

"Yalinikera, kwa nini shemeji yangu afanye yote hayo? Yaani upole wake, ucheshi wake na utulivu wake kumbe ni shetani mla nyama za binadamu? Kweli, simba mkimya ndiye mla nyama ama mbwa mnyenyekevu ndio mwizi wa mayai. Jamani hivi wema wangu wote, haya ndiyo malipo yangu?"

"Niliwaza, kwa nini walikataa kubaki na mgonjwa? Je, walifahamu kuwa haponi? Lengo lao kuu lilikuwa ni nini? Au walikuwa na lengo la shemeji yangu kumrithi marehemu ili yeye awe mke kwangu? Hivyo basi iliposhindikana akaamua kutunga na kutengeneza uongo wenye fitina ulioendana na ukweli kwa lengo kwamba, mke niliye nae sasa aweze kuchukia, aondoke kisha yeye shemeji yangu azamie?"

"Bwana Fujo, haya yalikuwa ni maumivu kwangu, ambayo yalikuwa ni mzigo mkubwa wa mawazo na mashaka. Je, unanipa ushauri gani rafiki yangu?" 

Laaa! Kusema kweli sikuwa na jipya la kumshauri bwana Tizo bali linimsisitiza amshitakie Mungu aliye hakimu wa haki. Hata hivyo nilimkubusha usemi usemao "MFADHILI MBUZI ...............BINADAMU............

=MWISHO=



 




No comments: